Mawaziri wa Afya na wadau wengine wa afya wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi
zilizo Kusini mwa Afrika (SADC), leo
wanakutana kwenye mkutano wa dharura kuzungumzia hatua za kudhibiti mlipuko wa
ugonjwa wa Ebola.
Mkutano huo unafanyika jijini
Johannesburg, Afrika Kusini una lengo la
kutoka na maazimio ya pamoja ya jinsi ya kukabili mlipuko wa ugonjwa huo ulioenea Magharibi mwa
Afrika ambao umeua mamia ya watu.
Tanzania ni miongoni mwa nchi
zinazoshiriki mkutano huo ikiwakilishwa na Naibu Waziri wa Afya, Dk Steven
Kebwe ambaye ameshawasili nchini humo.
Msemaji wa Wizara ya Afya, Nsachris
Mwamwaja alisema Naibu Waziri
atakaporejea nchini, atatoa taarifa ya yaliyojiri na hatua walizoafikiana
kuchukua kuthibiti ugonjwa huo.
“Ni kweli kuna mkutano huo, na sisi kama
wanachama wa SADC, tunahudhuria, Naibu Waziri tayari yupo huko akirejea
tutautaarifu umma yaliyojiri,” alisema Mwamwaja.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Sekretarieti
ya SADC, mkutano huo wa dharura, unafanyika leo jijini Johannesburg, Afrika
Kusini. Shirika la Afya Duniani (WHO), na wadau wengine wanashiriki.
“Lengo la mkutano huo ni kuja na nguvu ya
pamoja ya nini cha kufanya kudhibiti mlipuko wa ugonjwa huo, ambao unaendelea
kuangamiza maisha ya watu,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Alisema mkutano huo, utatoka pia na
maazimio ya pamoja ya mawaziri hao jinsi
ya kudhibiti ukanda wa SADC, dhidi ya ugonjwa huo.
Ugonjwa huo usio na tiba wala chanjo hadi
sasa umekumba nchi za Guinea, Liberia, Sierre Leone na Nigeria. Umesababisha
vifo vya zaidi ya watu 800 wakiwemo pia wataalamu na watafiti wa ugonjwa huo.
Hivi karibuni, serikali ilitoa hadhari
kuhusu ugonjwa huo na kusema imesambaza wataalamu wake kwenye mipaka nchi nzima
kuukabili endapo utaibuka.
Alisema wataalamu wa afya wataendelea
kutoa elimu ya afya juu ya ugonjwa huo ambao haujaripotiwa kuingia nchini.
Dalili za ugonjwa wa Ebola ni pamoja na
homa kali ya ghafla, kulegea mwili, maumivu ya misuli, kuumwa kichwa na kupatwa
na vidonda kooni.
Baada ya dalili hizo mgonjwa hutapika,
kuharisha, figo kushindwa kufanya kazi, kupatwa na vipele mwilini na kutokwa na
damu sehemu zote mwilini zenye matundu na mwisho ni kifo.
Dalili hizo huonekana baada ya siku mbili
hadi 21, ya mtu kupatwa na maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo.
No comments:
Post a Comment