Mshitakiwa
anayekabiliwa na kesi ya kuwa mwanachama wa kundi la kigaidi la Al Shabaab,
Mussa Mtweve, amepelekwa kwa Mkurugenzi
wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwa ajili ya mahojiano.
Hakimu Mkazi, Emilius Mchauru alitoa amri
hiyo jana baada ya kukubali ombi la upande wa Jamhuri wakati kesi hiyo
ilipotajwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Akiwasilisha ombi hilo, Wakili wa
Serikali Aldo Mkini alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na
DCI ameomba Mtweve apelekwe ofisini kwake kwa ajili ya mahojiano.
Hakimu Mchauru alikubali ombi hilo na
kuahirisha kesi hadi Agosti 18, mwaka huu itakapotajwa tena.
Mbali na Mtweve washitakiwa wengine
katika kesi hiyo ni Ally Rashid, Shaban Waziri na Faraji Ramadhani.
Inadaiwa
kati ya Januari 11, mwaka juzi na Septemba 16, mwaka jana, eneo la
Kibaoni, Dar es Salaam, Rashid alisajili watu hao (washitakiwa wenzake) kuwa
wanachama wa kundi hilo.
Alidai katika siku hizo, walikamatwa kwa
kuwa wanachama wa kundi la kigaidi la Al Shabaab nchini. Kundi hilo linafanya
shughuli zake Kenya na Somalia.
Washitakiwa hao wanaendelea kusota
rumande kutokana na mashitaka yao kutokuwa na dhamana.
No comments:
Post a Comment