WAJUMBE BUNGE LA KATIBA WAIVAA TUME YA JAJI WARIOBA


Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wamewajia juu waliokuwa Wajumbe wa Kamati ya Kukusanya Maoni ya Katiba wakidai kuwa kazi yao ilishaisha, hivyo kuendelea kujadili masuala kuhusu Rasimu ya Katiba si sahihi.
Baadhi ya wajumbe hao walitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti jana, wakati wakichangia Azimio la Kufanyia Marekebisho ya Kanuni za Bunge Maalumu iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge Maalumu, Pandu Ameir Kificho.
Mjumbe Dk Hamisi Kigwangwala, ambaye ni Mbunge wa Nzega, alisema ni vyema Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta akashauri wajumbe wa Tume hiyo  ambao ni wazee wenzake kwamba jukumu lao limeisha na kwa uungwana waachie Bunge Maalumu lifanye kazi yake.
“Wajumbe wale kazi yao ilishaisha, lakini kila siku wanakosoa, mara midahalo, makongamano. Wazuiwe kufanya hivyo, hata waambiwe tu kibinadamu maana hata sisi hatukuwaingilia wakati wanaendesha mchakato wao.
“Wanatuponda sana kana kwamba hakuna cha kujadili, kama ni hivyo zile siku 70 zilikuwa za nini?,” Alihoji.
Naye Dk  Zainabu Gama, alisema kazi ya Tume ya Katiba ilishaisha na kwamba kwa wanaopiga kelele nje ya Bunge Maalumu la Katiba watakuwa na lao jambo nyuma ya pazia.
Mjumbe Hamad Rashid Mohammed, ambaye pia ni Mbunge wa Wawi (CUF), alisema kwa taratibu za mabunge jambo lolote likishawasilishwa bungeni linakuwa chini ya mamlaka ya Bunge, ambalo nalo linafanya kazi kwa niaba ya wananchi.
Dk Pindi Chana akichangia, alisema ambao hawajarudi bungeni hawawatendei haki Watanzania.
Kwa upande wake John Cheyo alisema hakuna haraka ya kupata Katiba na kwamba ni vyema umakini mkubwa ukawepo katika kuhakikisha inapatikana Katiba bora.
“Tusiharakishe suala la Katiba, kama tunaona gharama basi tujaribu fujo, ghasia na kutoelewana, hiyo ndiyo gharama zaidi,” alisema.

No comments: