Ujenzi wa mradi
wa kituo kikubwa cha viwanda na biashara katika eneo la Kurasini jijini Dar es
Salaam unatarajiwa kuanza hivi karibuni.
Matarajio hayo
yanatokana na serikali kutenga Sh bilioni 53 zitakazotumika kuwalipa fidia
wakazi wa eneo hilo kupisha ujenzi wa kituo hicho kijulikanacho kama Tanzania
China Logistics.
Waziri wa
Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda aliwaambia waandishi wa habari jana
jijini Dar es Salaam kwamba serikali imeshaipatia Mamlaka ya Ukanda Maalumu ya
Uwekezaji (EPZA) mchakato wa ulipaji uanze mara moja kabla ya ujenzi kuanza.
Katika mradi
huo, serikali ya China itawakilishwa na kampuni ya Yiwu Pan-Africa
International Investment Corporation na Tanzania itawakilishwa na EPZA. Zaidi
ya wananchi 1,020 wanatakiwa kuhama eneo
hilo la mradi.
Ujenzi wa mradi
huo utagharimu Dola za Marekani milioni 400 ambazo ni sawa na Sh bilioni 660
ambazo zitagharimiwa na serikali ya China. Tanzania imetoa ardhi na kulipa
fidia kwa wakazi wa maeneo hayo.
Eneo la mradi
huu lenye ukubwa wa ekari 60.4 limetengwa katika kata ya Kurasini jijini hapa
na linahusisha mitaa ya Shimo la Udongo, Mivinjeni na Kiungani. “Tunatarajia
kituo hicho kuwa kikubwa Afrika ya Mashariki na Kati,” alisema Waziri.
No comments:
Post a Comment