Chama Cha
Mapinduzi(CCM) kimewabana mawaziri na wabunge wake wasiohudhuria
shughuli za Bunge Maalumu la Katiba.
Moja ya hatua
iliyochukuliwa na chama hicho tawala ni kupunguza idadi yao kwenye ziara
ya Rais Jakaya Kikwete aliyoianza jana mkoani Morogoro.
Vilevile
mawaziri wote wasiokuwa na shughuli za msingi au za lazima wametakiwa lazima
kuhudhuria vikao vya kamati na mjadala wa bunge hilo tofauti na sasa wengi
ambapo wengi wao wamekuwa hawahudhurii kabisa au wanahudhuria mara chache.
Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu(NEC) ya CCM, Nape Nnauye alibainisha hayo
wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka kufahamu msimamo wa
Kamati Kuu (CC) kuhusu mawaziri na wabunge
wasiohudhuria
bunge hilo.
Nnauye alikuwa
akitoa maelezo ya kilichojiri kwenye CC iliyokutana juzi mjini hapa chini ya
Mwenyekiti wa chama hicho, Jakaya Kikwete kujadili Maendeleo ya Mchakato wa
mabadiliko ya Katiba nchini ndani ya nje ya bunge hilo.
Akizungumzia
kilichojiri kwenye CC ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Katibu huyo wa Itikadi
alisema imeridhishwa na juhudi za vyama vya siasa na wadau katika kujenga na
kuimarisha maridhiano na mshikamano kwa lengo la kupata muafaka, lakini
imesikitishwa kuvunjika kwa mazungumzo kati ya CCM na vyama vya upinzani
vinavyounga Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi) ambavyo ni CUF, Chadema na NCCR
Mageuzi yaliyokuwa yanasimamiwa na Msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji
Francis Mutungi yakiwa na lengo la kupata maridhiano.
“Kamati Kuu
imepokea na kuridhishwa na taarifa kuhusu juhudi zinazofanywa na TCD(Baraza la
Demokrasia nchini) na vyama vinavyounda TCD katika kutafuta muafaka wa kisiasa
kwa lengo la kuimarisha amani, utulivu, mshikamano na kuaminiana kati ya wadau
mbalimbali na hasa kati ya vyama vya siasa”, alisema.
Kamati Kuu hiyo
imemuagiza Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana pamoja na kazi nzuri
anayofanya kukiwakilisha chama hicho kwenye vikao vya maridhiano kuendelea
kukutana na vyama hivyo na wadau wengine katika kufanikisha lengo la maridhiano
ili kupatikane katiba mpya.
Pamoja na hayo
CC imeridhishwa na mwenendo wa Bunge la Katiba na majadiliano na upigaji kura
katika kamati hizo za bunge hilo.
“Kamati kuu imeridhishwa namna wajumbe wa
Bunge Maalumu wanavyoshiriki katika kujadili na kujenga hoja na
wanavyoshughulikia tofauti za kimtazamo na kimawazo katika vikao vyao na
uhitimishaji wa majadiliano kwa kura…CC inawahimiza wajumbe wa bunge kushiriki
kwenye mijadala kwa kutanguliza maslahi mapana ya taifa na kuipatia nchi katiba
inayotarajiwa na watanzania wote,”alisema.
No comments:
Post a Comment