Jeshi la
Wananchi Tanzania (JWTZ) limeendelea kung’ara kimataifa, ambapo jana jeshi hilo
lilitamkwa kuwa miongoni mwa majeshi ya nchi za Afrika, yatakayounda Jeshi la
Kulinda Amani Afrika.
Taarifa za ndani
kutoka Mkutano wa Kimataifa wa Wakuu wa Nchi na Serikali zaidi ya 50 za Afrika
na Marekani, ambao umehudhuriwa pia na Rais Jakaya Kikwete, zimeeleza kuwa moja
ya kazi za jeshi hilo, itakuwa kuwa tayari wakati wowote, kukabiliana na tishio
la kiusalama ndani ya Afrika.
Taarifa za
Shirika la kimataifa la habari la Reuters, zilizotolewa jana, zilieleza kuwa
Serikali ya Marekani katika mkutano huo uliomalizika juzi, imejipanga kutumia
Dola za Marekani milioni 110 kila mwaka kwa miaka mitatu mpaka mitano ijayo,
kusaidia jeshi hilo kufanya kazi kwa haraka katika maeneo yanayokabiliwa na tishio
la usalama na amani Afrika.
Hivi karibuni
vikao vya JWTZ vinavyolinda amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Congo (DRC), vilitajwa kuwa miongoni mwa vikosi bora 35 vya majeshi ya nchi
mbalimbali duniani, vinavyokubalika kwa kuwa na ufanisi wa hali ya juu, uwezo
mkubwa wa kupigana na vilivyofundishwa vizuri.
Mtandao wa
Kimataifa wa Imgur Via Distractify, ulieleza kuwa Tanzania ni nchi pekee ya
Afrika, yenye jeshi ambalo ni
miongoni mwa majeshi bora 35 duniani.
Mwandishi, Micky
Wren aliandika katika mtandao huo kuwa,
majeshi hayo, ikiwemo JWTZ yamefundishwa kwa kiwango cha juu, yana
silaha za kisasa na yameandaliwa vizuri kwa ajili ya operesheni ngumu za
kijeshi.
Pia, majeshi
hayo yalitajwa kuwa yenye uwezo wa kukabiliana na adui katika mazingira yoyote,
kuanzia kumaliza uhuni wa utekaji
hadi kusambaratisha wahalifu wenye uwezo mkubwa.
Mwandishi huyo
alitaja majeshi hayo katika orodha ambayo haikupangwa kwa mtitiriko wa uwezo wa
kijeshi, ambapo mbali na JWTZ mengine ni Kikosi cha Seal cha Jeshi la Maji la
Marekani na Kikosi cha SAS cha Jeshi la Uingereza.
Kipo pia Kikosi
cha Huntsmen Corps cha Majeshi Maalumu ya Denmark, Majeshi Maalumu ya Ufaransa,
Kikosi cha MARSOC, Majeshi Maalumu ya Taiwan ambayo yanatumia kinga za usoni
zisizoweza kuingiliwa na risasi na Kikosi cha Irish Army Rangers cha Jamhuri ya
Ireland.
Vingine ni
Gendarmerie cha Serbia, Kikosi Maalumu cha Kukabiliana na Ugaidi cha JTF2 cha
Canada, Majeshi Maalumu ya Uholanzi, Kikosi cha SBS, Majeshi Maalumu ya Jamhuri
ya Korea na Majeshi Maalumu ya Ufaransa.
Pia, yapo
Majeshi Maalumu ya Ubelgiji, Kikosi cha MJK cha Norway, Canadian Joint Response
Unit cha Canada, Majeshi Maalumu ya Norway, Kikosi cha French Commando Marine,
Majeshi Maalumu ya New Zealand, Kikosi cha Norwegian Armed Forces Special
Command na Kikosi cha Polish Grom cha Poland.
Vingine ni
Kikosi cha US Army Special Forces Sniper with Remington Modular Sniper Rifle,
Majeshi Maalumu ya Marekani, Majeshi Maalum ya Indonesia, Majeshi Maalum ya
Romania na Kikosi cha SASR cha Australia.
Kikosi cha KSK
cha Ujerumani, Majeshi Maalumu ya Ujerumani, Majeshi Maalumu ya Israel –
Shayetet 13, Majeshi Maalumu ya Urusi – Spetsnaz, Majeshi Maalum ya Austria –
Jagdkommando, Majeshi Maalumu ya Iraq, Majeshi Maalumu ya Ujerumani ya SEK-M na
Majeshi Maalumu ya Peru.
Maofisa wa
Serikali ya Marekani, wamekaririwa na Reuters wakieleza kwamba mbali na
Tanzania, majeshi mengine yatakayounda jeshi hilo yanatoka nchi za Senegal,
Ghana, Ethiopia, Rwanda na Uganda.
“Tumeshuhudia
kwa muda mrefu sasa majeshi ya nchi za Afrika, yakifanya kazi kwa weledi katika
maeneo yenye migogoro,” ilisema Reuters
ikimkariri ofisa mmoja wa Serikali ya Marekani.
Ofisa huyo
alisema pamoja na mafanikio ya majeshi hayo ya Afrika, bado kumeendelea
kujitokeza changamoto ya kusaidia vikosi vya majeshi hayo, kuingilia kati
sehemu zenye migogoro kwa haraka zaidi, pamoja na namna ya kujilinda na
kujikimu wakiwa katika majukumu hayo ya kimataifa.
Kutokana na
changamoto hizo, fedha hizo zinazofikia Dola milioni 550 baada ya miaka hiyo mitano,
zinatarajiwa kuanza kutolewa mwanzoni mwa mwaka wa fedha wa Marekani unaoanza
Oktoba mwaka huu, na zitapelekwa moja kwa moja, kusaidia utendaji wa haraka wa
jeshi hilo, katika maeneo yanayokabiliwa na tishio la kuibuka kwa migogoro.
No comments:
Post a Comment