Ofisa ya Takwimu
ya Taifa (NBS) imesema mfumko wa bei wa mwezi Julai, umeongezeka kidogo kutoka
asilimia 6.4 ilivyokuwa Juni hadi
asilimia 6.5.
Hata hivyo,
alisema bei za bidhaa za vyakula,
hazikupanda licha ya kuwepo malalamiko kutoka kwa wananchi, kuwa bei za vyakula
zilipanda maradufu mwezi uliopita.
Mwezi uliopita
Waislamu ambao walikuwa kwenye Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani,
walilalamikia kupanda kwa bei za vyakula, hasa wanavyotumia kupika futari kama
magimbi, muhogo, viazi, maharage na tambi, kuwa bei yake ilipanda maradufu.
Lakini, NBS
imesisitiza kuwa vyakula vinavyotumiwa na Watanzania wengi, bei zake
hazikupanda, bali bei za vyakula ambavyo havitumiwi na watu wengi, ndivyo bei
yake ilipanda, lakini haikuathiri ukokotoaji wa mfumuko wa bei.
Mkurugenzi wa
Sensa na Takwimu za Jamii wa NBS, Ephrahim Kwesigabo alisema jana kuwa
kupanda kwa mfumuko wa bei mwezi Julai, kunamaanisha kuwa kasi ya upandaji wa
bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Julai, imeongezeka kidogo,
ikilinganishwa na mwezi ulioshia Juni.
"Ila
mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi, umebaki kuwa asilimia
8.1 mwei Julai kama ilivyokuwa mwezi Juni," alisema Kwesigabo wakati
akizungumza na waandishi wa habari.
Akizungumzia
mfumko wa bei kwa bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula, Kwesigabo
alisema badiliko la fahirisi za bei za bidhaa za vyakula nyumbani na
migahawani, limepungua hadi asilimia 7.9 mwezi Julai kutoka asilimia 8.7 mwezi
Juni.
Alisema fahirisi
za bei kwa bidhaa zisizo za vyakula, limeongezeka hadi asilimia 4.9 kutoka
asilimia 4.8 mwezi Juni. Alitaja bidhaa hizo kuwa ni bia bei imepanda kwa
asilimia 4.4, sigara asilimia 2.1, kodi ya pango asilimia 2.5 na mkaa asilimia
1.2.
Alisema mfumuko
wa bei, ambao haujumuishi vyakula na nishati kwa mwezi Julai, umepungua hadi
asilimia 3.2 kutoka asilimia 3.5 ilivyokuwa Juni.
Kuhusu thamani
ya Shilingi ya Tanzania kwa mwezi
Julai, alisema uwezo wa Shilingi 100 katika kununua bidhaa na huduma, umefikia
asilimia 67 na senti 04.
Akizungumza
mfumuko wa bei kwa kipimo cha mwezi, Kwesigabo alisema umeongezeka kwa asilimia
0.1, ikilinganishwa na kupungua kwa asilimia 0.6 kama ilivyokuwa Juni. Lakini
alisema fahirisi za bei, zimeongezeka hadi 149.16 Julai kutoka 148.98 mwezi
Juni.
No comments:
Post a Comment