Serikali imeongeza nguvu ya kukabiliana
na mlipuko wa ugonjwa wa ebola iwapo utatokea, kwa kuwapima wasafiri na wageni
wanaoingia nchini kupitia viwanja vikubwa vitano vya ndege.
Vipimo hivyo vitafanywa ili kubaini iwapo
wana vimelea vya ugonjwa huo, kwa kutumia mashine za thermoscan
zinazotarajiwa kuingia nchini wiki mbili zijazo.
Hayo yalibainishwa Dar es Salaam jana na
Naibu Waziri wa Afya, Dk Kebwe Stephen Kebwe alipokuwa akizungumzia ripoti ya
mkutano wa dharura kwa mawaziri wa
Afya na wadau wengine wa afya wa nchi
wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi zilizo kusini mwa Jangwa la
Sahara (SADC), kuhusu ebola.
Dk Kebwe alisema katika mkutano huo wa
dharura uliofanyika Agosti 6, mwaka huu, Afrika Kusini, ulimalizika kwa
kuwekeana malengo na maazimio ya kutekeleza kwa haraka ili kukabiliana na
mlipuko wa ugonjwa huo, ambao umeathiri zaidi nchi za Afrika Magharibi.
“Tumekubaliana jambo ili liwe nyeti na
tunachukua hatua za haraka kuudhibiti na kuwaelimisha wananchi, mlipuko wa
kipindi hiki ni mkubwa, haujawahi kutokea duniani”, alisema Dk Kebwe.
Alisema ugonjwa huo usio na tiba wala
chanjo hadi sasa umeshazikumba nchi za Guinea, Liberia, Sierre Leone na Nigeria
na umesababisha vifo vya zaidi ya watu 1,000, wakiwemo pia wataalamu na
watafiti wa ugonjwa huo.
Pia umezikumba nchi za Mashariki ya Kati,
ikiwemo Saudia Arabia na Falme za Kiarabu kwenye mji wa Dubai.
Akizungumzia hatua zilizochukuliwa na
Tanzania kukabiliana na ugonjwa huo, Dk Kebwe alisema wiki mbili zijazo,
mashine za thermoscan zilizoagizwa
kutoka Afrika Kusini zitawasili nchini na kusambazwa kwenye viwanja vitano vya
ndege.
Viwanja hivyo ni pamoja na cha Kimataifa
cha Julius Nyerere (JNIA), cha Kilimanjaro (KIA), wa Mwanza, Zanzibar na Mbeya.
Alisema mashine hizo zitakuwa zikiwapima
wasafiri na wageni wote wanaoingia nchini kutokea nchi za Afrika Magharibi na
kwengineko, ili kubaini kama wana vimelea vya ugonjwa huo, ili iwe rahisi
kutibu na kuepusha maambukizi kwa wengine.
“Ugonjwa huu hauna kinga wala chanjo na
unasambaa kwa haraka sana, hivyo kama tutabaini wenye vimelea au ugonjwa huo
mapema, tunaweza kuwatibu kwa maradhi ya awali na kuepusha kuambukiza
wengine,”alisema Dk Kebwe.
Alisema serikali kwa kutambua uzito wa
ugonjwa huo, umechukua hatua za haraka kwa kupeleka wataalamu wa afya 17,000
kwenye mipaka yote nchini pamoja na vifaa tiba kama vile dawa, buti, miwani,
maski, aproni pamoja na nguo za kujikinga.
Aidha, msambazaji wa vifaa hivyo ana
taarifa na iwapo vitahitajika vingine ndani ya saa 48 hadi 72, vifaa hivyo
vitakuwa vimeshaagizwa nje ya nchi na kuingia.
Ingawa ugonjwa huo haujaingia nchini, Dk
Kebwe alitoa mwito kwa wananchi kuchukua tahadhari na kutoa taarifa na kwenda
kwenye kituo cha afya iwapo wataona dalili za ugonjwa huo, ambazo ni pamoja na
homa kali ya ghafla, kulegea mwili, maumivu ya misuli, kumwa kichwa na kupatwa
na vidonda kooni.
Baada ya dalili hizo, mgonjwa hutapika,
kuharisha, figo kushindwa kufanya kazi, kupatwa na vipele mwilini na kutokwa na
damu sehemu zote mwilini zenye matundu na mwisho ni kifo. Na kwamba dalili hizo
huonekana baada ya siku mbili hadi 21, ya mtu kupatwa na maambukizi ya virusi
vya ugonjwa huo.
No comments:
Post a Comment