Mbunge wa
Maswa Magharibi, John Shibuda (Chadema), amesema hatagombea ubunge kupitia
Chadema katika Uchaguzi Mkuu ujao, kwa
kuwa amechoshwa na kauli za vitisho na kejeli dhidi yake, zinazotolewa
na baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho.
Amesema
hayo jana kwa nyakati tofauti, wakati akizungumza na wazee wa Mji wa Maswa na
Malampaka wilayani humo, alipokuwa akijibu swali lao kuhusu hatima yake ya
kisiasa ndani ya Chadema, baada ya chama hicho kutishia kumfukuza.
Alipoulizwa
na wazee ni chama kipi atagombea ubunge katika Uchaguzi Mkuu ujao, alisema wakati ukifika atasema kwani kwa
sasa bado anatimiza
wajibu wake wa kutetea wapiga kura wake ambao wengi
wao ni
wakulima na wafugaji na yuko tayari kufukuzwa ndani ya Chadema kwa kuwatetea wao.
Alisema
kuwa aliingia katika chama hicho kwa hiari yake baada ya kukataa dhuluma alizodai kufanyiwa
na CCM na kudhani ndani ya Chadema kuna demokrasia na ukombozi wa kweli, lakini
alichokikuta ni tofauti kwani kila siku amekuwa akipata misukosuko kutoka ndani
ya chama hicho.
"Mie
niliingia Chadema kwa hiari yangu baada ya kuona dhuluma zilizokuwa ndani ya CCM, chama
kilichonilea kisiasa, nikaona heri
niende
Chadema ambako nilidhani kuna demokrasia na ukombozi wa kweli, lakini
nilichokikuta humo ni tofauti kwani kila siku wazee wangu
mnasikia
napata misukosuko isiyo na maana," alisema.
Alisema
pamoja na misukosuko hiyo, amekuwa kimya muda mrefu kiasi kwamba kuna wakati
vijana ndani ya chama hicho walimtukana matusi, wakatoa maneno mbalimbali ya
kumdhalilisha kwa kumwita ‘Msaliti’ na ‘Pandikizi wa CCM’, huku viongozi wa
ngazi za juu wa chama hicho, wakikaa kimya bila kuchukua hatua.
"Pamoja
na shutuma zote zinazotolewa juu yangu na kupachikwa majina mbalimbali kuwa mie ni ‘Msaliti’
mara ni ‘Pandikizi la CCM’, lakini hata siku moja sijawahi kuitwa katika Kamati Kuu ya Chadema na
kuhojiwa.
“Nimekuwa
nikitukanwa hadharani na vijana wa Chadema mbele ya viongozi wa juu wa chama, hawachukui hatua… mie mtu mzima hapo
natafsiri kuwa wametumwa na viongozi hao ili kunifanyia fitna hizo,"
alisema.
Akizungumzia
tuhuma zilizotolewa juu yake za kukiuka msimamo wa kutohudhuria vikao vya Bunge
Maalumu la Katiba, uliowekwa kwa wajumbe wa Bunge hilo kutoka kundi la Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa), alisema tuhuma hizo hazina msingi wowote kwani
hajahudhuria kikao hicho
wala hakuchukua posho.
Alisema
alifika mjini Dodoma akitokea Dar es Salaam akiwa njiani kwenda katika Jimbo
lake la Maswa Magharibi na alipita bungeni
kufuatilia fedha za matibabu kutokana na kusumbuliwa na mguu.
Akiwa
bungeni Shibuda alisema alijaza fomu za matibabu kwa kuwa wabunge wanatibiwa na
Serikali kupitia Ofisi ya Bunge kwa kipindi chote cha uhai wa ubunge wao.
"Mie
ni kweli nilipita Dodoma nikitokea Dar es Salaam kuja huku jimboni na nilifika
Ofisi za Bunge ili nipatiwe fedha za matibabu kwani nasumbuliwa na mguu na siye
tunatibiwa na Serikali kupitia Ofisi ya Bunge kwa kipindi chote cha ubunge sasa
kosa langu la kuitwa msaliti hapa ni lipi?
“Hata
hiyo posho wanayodai nimeichukua iko wapi? Labda wameweka katika akaunti ila
mie nasisitiza sijachukua posho wala kuhudhuria kikao hicho," alisema.
Alisisitiza
kuwa tangu habari hizo zianze kuandikwa na kutangazwa katika vyombo vya habari, hajawahi
kuulizwa na kiongozi yeyote wa Chadema,
isipokuwa amesikitishwa na kauli ya Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu,
kutishia kumfukuza ndani ya chama kwa usaliti.
"Uongozi
ni kutanguliza hekima na busara katika kufikia uamuzi, uongozi si Magereza na hata Magereza wafungwa wana
haki zao, Tundu Lissu
amekuwa nani katika nchi hii… anaongea kama kasuku hafanyi utafiti anakurupuka na
kuongea na kutoa matamko? Mie nitamtaka athibitishe tuhuma hizo anazozitoa
dhidi yangu. Nasema Chadema si baba wala mama yangu," alisema.
Alisisitiza
kuwa amechoka kusikia hukumu dhidi yake kila siku kupitia vyombo vya habari kutoka
kwa viongozi wake wa Chadema, huku
akitoa mfano kuwa alipounga mkono nyongeza ya posho ya Bunge, aliitwa
‘Msaliti’, lakini leo wabunge wote wakiwemo wa Chadema waliogomea wanachukua
posho hiyo.
"Wazee
wangu niliposema bungeni posho iongezwe, niliitwa mie ‘Msaliti’ na wabunge wa
Chadema lakini leo kila mmoja muulizeni hata huyu Kasulumbayi (Sylvester, Mbunge wa
Maswa Mashariki, Chadema), ambaye tunaye hapa kwenye kikao kama hachukui posho
hizo.
“Hata
huyo Tundu Lissu anayeongea sana anachukua, hata Mbowe (Freeman, Mwenyekiti wa
Chadema) alikataa gari la Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, lile la
Serikali lakini hadi leo analitumia… mbona yeye haitwi ‘Msaliti’?” Alihoji
Shibuda.
Akizungumzia
uhusika wake katika kundi la Ukawa, Shibuda alisema kuwa yeye si sehemu ya kundi
hilo na wala hajawahi kuelimishwa kuhusu kundi hilo, bali anakumbuka kuwa
kupitia viongozi wa juu wa vyama vya Chadema, CUF na NCCR –Mageuzi,
walikubaliana katika kikao kuwa wabunge wa vyama hivyo watoke bungeni na
wasishiriki vikao hivyo.
"Muislamu
hawezi kutetea Uislamu kama hajui nguzo saba za Uislamu na pia huwezi kuwa
Shekhe bila kupitia Madrasa na hata katika Ukristo,
huwezi
kuutetea Ukristo kama hujui Biblia na hukusoma mafundisho… na mie siwezi kuwa
Ukawa wakati sijaelimishwa kuhusu kundi hilo,” alisema.
Lissu
alipopigiwa simu na gazeti hili ili atoe ufafanuzi, alisema taarifa kwamba
Shibuda amepokea posho katika Bunge Maalum la Katiba, alizipata kwa waandishi
wa habari.
Alipoulizwa
kama alijaribu kuthibitisha taarifa hizo, alisema taarifa hizo zimeelezwa kwa
waandishi wa habari na Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, Yahaya Khamis Hamad.
Lissu
alisisitiza kwamba Shibuda alisaini posho mara moja, na ndio maana Katibu wa
Bunge hilo, aliwaambia waandishi wa habari na yeye kupata taarifa hizo kupitia
magazeti.
Kuhusu
Shibuda kutogombea Ubunge kupitia Chadema, alisema angemshangaa kama asingetoa ujumbe huo, kwani
amekuwa akienda kinyume na msimamo wa wenziwe tangu siku ya kwanza ya kuanza
kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Shibuda
kwenda kinyume na wenzake hajaanza leo, ameanza siku ya kwanza tu wakati Rais
Jakaya Kikwete alipozindua Bunge na hajabadilika, kwa hiyo kutamka msimamo wake
ni sawasawa tu,” alisema Lissu.
Alisema
Shibuda anajua mambo yake bungeni hivyo wangeshangaa kama bado angekuwa na nia
ya kugombea nafasi yoyote kupitia chama hicho.
No comments:
Post a Comment