WANAWAKE 1,600 WAACHIKA ZANZIBAR KATIKA MWAKA MMOJA


Takwimu za Mahakama ya Kadhi Zanzibar, zimeonesha kuwa zaidi ya talaka 1,600 zimetolewa Zanzibar kati ya 2012 na 2013, huku wanawake wengi wakitelekezwa bila kupatiwa haki zao baada ya kutengana na wenza wao.
Akizungumzia hali hiyo juzi mbele ya waandishi wa habari, Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Hassan Othman Ngwali, alisema kwa sasa peke yake kuna kesi 1,917 za talaka  mbele ya Mahakama sita za Unguja.
Mbali na kuwa na kesi hizo, Ngwali alisema wanawake wamekuwa waathirika wakuu baada ya kuvunjika kwa ndoa, kwa kuwa hakuna hukumu ya kesi zilizopita, ambayo haki ya mgawanyo wa mali kwa wanandoa imetolewa.
Alitaja baadhi ya sababu zinazochangia kuwepo kwa wingi wa talaka Zanzibar, kuwa ni pamoja na wanandoa wenyewe kukosa mafunzo ya ndoa na majukumu yake kwa ujumla.
“Moja ya tatizo la kuvunjika kwa ndoa katika jamii, ni wanandoa kukosa elimu ambayo itawafanya kujua haki na faida zinazopatikana katika ndoa,” alisema.
Alisema Ofisi ya Mahakama ya Kadhi imeanza kutoa elimu kwa makadhi wote kuhusu haki za wanandoa katika kipindi chote wanapokuwa kwenye ndoa.
Naye Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar, Bakari Mshibe, alisema marekebisho ya Sheria ya Mahakama ya Kadhi, yapo katika hatua za mwisho kuwasilishwa mbele ya Baraza la Wawakilishi.
Alitaja baadhi ya mambo yaliyofanyiwa marekebisho kwa lengo la kuimarisha Mahakama hizo, kuwa ni pamoja na kutoa uwezo wa kumshurutisha mwanamume kutoa matunzo ya mtoto wakati ndoa inapovunjika.
“Moja ya mambo yaliyopewa kipaumbele katika marekebisho ya Sheria ya Mahakama ya Kadhi, ni kuwabana wazazi ambao hawatoi matunzo kwa watoto wakati ndoa inapovunjika,” alisema.
Wanaharakati wengi Zanzibar, wanataka kuwepo kwa marekebisho makubwa katika Sheria hiyo ya Mahakama ya Kadhi, hasa katika mgawanyo wa mali kwa wanandoa wakati wanapotengana.

No comments: