UNGA WA LISHE NI HATARI KWA WATOTO


Mchanganyiko usiozingatia makundi matano ya vyakula, unaotengenezwa na wajasiriamali au nyumbani kwa ajili ya unga wa watoto maarufu ‘Lishe’, una athari za kiafya kwa watoto wachanga na walio chini ya miaka mitano.
Daktari Bingwa wa Watoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Augustine Massawe, amesema unga huo ni hatari kwa sababu mchanganyiko wake si muafaka kwa watoto.
Dk Massawe alikuwa akitoa mada kwenye semina ya waandishi wa habari kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Unyonyeshaji Maziwa ya Mama.
Alisema kwanza utengenezaji wa unga huo hauzingatii vipimo maalumu, wala makundi ya virutubisho anavyopaswa kupata mtoto katika mlo mmoja, ambavyo ni wanga, protini, vitamini, mafuta na madini.
Massawe alikosoa utengenezwaji wa unga unaochanganywa  mahindi, mchele, ulezi, soya, mtama, karanga na dagaa.
“ Mchanganyo kama huu haukubaliki kwa sababu katika mchanganyiko wa aina hii, kuna orodha ya nafaka ambazo zina kirutubisho kimoja cha wanga na haziongezi virutubisho vingine.
“Mbaya zaidi katika mchanganyo kama huu, kila aina ya nafaka inayowekwa, ina muda wake wa kuiva na hautakuwa na ladha kwa mtoto zaidi ya kuleta ugumu katika mmeng’enyo wa chakula tumboni kwa mtoto,” alisema Dk Masawe.
Wataalamu wanashauri muandaaji wa chakula cha mtoto,  kupika unga wa aina moja ya nafaka, ukishaiva ndio aweke unga wa karanga ambazo zimesafishwa, ili kuondolewa fangasi zinazoleta sumu ya toxin inayoambukiza saratani ya ini.
Kwa mujibu wa ushauri huo, endapo karanga zitawekwa kwenye mchanganyo wa nafaka kama ilivyo kwa baadhi ya unga wa lishe, zina tabia ya kupungua katika kila hatua.
Karanga zimetajwa kupungua wakati wa kusaga mchanganyiko huo, ambapo hunata katika mashine, pia wakati wa kuchekecha unga, karanga hubaki katika kichekecho na wakati wa kupika, kutokana na kuwa na hulka ya kuungua kabla uji haujaiva, hubakia katika sufuria na hivyo kumkosesha mtoto protini na mafuta.
Baadhi ya athari ya mchanganyiko huo, ni watoto kufunga choo kutokana na chakula kushindwa kumeng’enywa, kuhara na kukosa vitamini.
Athari nyingine mbaya ni mtoto kuwa hatarini kupata saratani ya ini, kama karanga zilizochanganywa katika lishe, hazikuoshwa vizuri.
Massawe alipendekeza wazazi watumie aina moja ya nafaka kama mahindi ambayo yanatoa wanga, mafuta na nyuzi.
Aidha Mtaalamu kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), Neema Joshua alisema taasisi yake imekuwa ikifanya juhudi za kutoa elimu kwa jamii kuachana na aina hii ya michanganyo.
Alisema changamoto wanayokutana nayo katika kupambana na hali hiyo, inatokana na wajasiriamali kukwepa sheria kwa kutambulisha kuwa mchanganyiko huo ni muafaka kwa watoto, wagonjwa na wazee.
Neema alisema kumekuwapo na ongezeko la utapiamlo kwa watoto, unaosababishwa na vyakula vya aina moja na visivyokuwa na virutubisho kama wanga, protini, vitamini na mafuta.
Naye Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Gaudensia Simwanza, alisema Taasisi yake imekuwa ikifanya juhudi za kutoa elimu kwa wajasiriamali, ili watengeneze unga unaojumuisha makundi hayo matano ya vyakula. 
“Tumekuwa tukitoa elimu kwa wajasiriamali na baada ya hapo, tunasajili bidhaa zao kwa wale wanaozingatia muongozo wa TFDA na Taasisi ya Chakula na Lishe,” alisema.

No comments: