Wakala wa
Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) umebaini udanganyifu uliofanywa na walimu wa
shule za msingi na wazazi kughushi taarifa na kuongeza bei wakati wa kusajili
na kuwapatia wanafunzi vyeti vya kuzaliwa.
Hayo yalisemwa
jana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Rita,
Philip Saliboko (pichani) wakati wa uzinduzi wa utekelezaji mkakati wa usajili na
kuwapatia vyeti wanafunzi wa sekondari uliofanyika jijini hapa.
Alisema ni vyema
walimu wakaweka uzalendo mbele na kufuata maelekezo ya utoaji nyaraka kama
watakavyofundishwa na kuepuka vitendo vya udanganyifu kama vilivyofanywa na
baadhi ya walimu wa shule za msingi.
Aliongeza kuwa
Rita kwa kushirikiana na ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala inategemea
kuanza uandikishwaji kwa shule za sekondari za mkoa wa Dar es Salaam na
utafanyika chini ya mkakati wa usajili wa watoto walio na umri kati ya miaka
6-18 kwani watoto wengi wapo kwenye kundi hilo.
“Jumla ya shule
za sekondari 96 zitashiriki katika mkakati huu zenye jumla ya wanafunzi 53,028
na lengo ni kusajili na kutoa vyeti kwa wanafunzi 15,000,” alisema Saliboko na
kufafanua kuwa walimu watakusanya ada za vyeti kwa kila mtoto ya Sh 10,000 tu.
Ofisa Elimu
Msaidizi Manispaa ya Ilala, aliyekuwa mgeni rasmi Epifania Mtumbuka alisema
wazazi wanatakiwa kupeleka watoto wao kusajiliwa ili mtoto akimaliza kidato cha
sita na akipata nafasi ya kwenda nje awe na cheti cha kuzaliwa.
No comments:
Post a Comment