Chuo cha
Kimataifa cha Kampala (KIU) kimetangaza kutoa udhamini kwa wanafunzi 1,800
watakaojiunga kuanzia mwaka huu wa masomo kwa kuwalipia nusu ya ada.
Mpango huo wa
udhamini ambao umetajwa kuwa endelevu, umeelezewa na uongozi wa chuo kwamba
utakigharimu takribani Sh bilioni 2.5 kila mwaka kuutekeleza.
KIU ambacho
kimetoa nafasi 10 kwa kila wilaya kwa wanafunzi watakaojiunga nacho na kufanya
idadi ya wadhaminiwa kufikia 1,800, pia kimeshusha ada kutoka Sh milioni 2.8
hadi Sh milioni 1.6 kwa masomo ya jamii.
Uongozi wa chuo
hicho ulitoa taarifa hiyo jana Dar es Salaam
kwenye mkutano na wahariri wa vyombo vya habari na kusema ni mkakati
wake wa kuhudumia jamii ya Watanzania.
Makamu Mkuu wa
Chuo, Profesa Muhammad Ndaula alisema udhamini wa chuo hicho chenye uwezo wa
kudahili wanafunzi 6,000 mwaka huu, utazingatia ufaulu pamoja na wanafunzi
wasio na uwezo kiuchumi.
Alisema kwa kuwa
wanafanya kazi kwa karibu na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) pamoja na Bodi ya Mikopo
ya Elimu ya Juu (Heslb), alisema vigezo vya bodi katika kutoa mkopo pia
vitasaidia wao kubaini wanafunzi wenye uhitaji.
“Mpango unaanza
sasa na ni endelevu,” alisema Profesa Ndaula na kufafanua kwamba kwa
wanaochukua kozi za miaka mitatu, udhamini ni kwa asilimia 50 na kwa wenye kozi
za miaka minne watadhaminiwa kwa asilimia 40.
Kuhusu kupunguza
ada, Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano, Thomas Somme alisema baada ya kuona
Watanzania wengi wanashindWa kupata elimu kwa sababu ya ada kubwa, wameamua
kupunguza kwa kiwango hicho kikubwa.
Alipoulizwa kama
upunguzaji ada ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa TCU wa ada elekezi kwa
vyuo, Somme alisema wamezingatia mantiki ya biashara pamoja na utoaji huduma
kwa jamii.
Machi mwaka huu,
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alizindua mfumo wa
gharama halisi za vyuo vikuu nchini ulio chini ya TCU. Alitaka taasisi za elimu
ya juu kutafuta vyanzo vingine vya fedha badala ya kutegemea serikali na ada.
No comments:
Post a Comment