Unaweza kusema ni mikasa imeaanza kumwandama Mchungaji Getrude
Rwakatare baada ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi kuvunja nyumba nne
zilizojengwa ndani ya kiwanja namba 314 zilichopo eneo la Mbezi Beach, jijini
Dar es Salaam zinazomilikiwa na mchungaji huyo kwa tuhuma kuwa alivamia eneo
hilo.
Kazi hiyo ya ubomoaji, ilitekelezwa chini ya ulinzi mkali
wa Polisi na iliendeshwa kwa pamoja na maofisa wa Ardhi kutoka wizarani na Manispaa ya Kinondoni, waliodai
wamepewa agizo hilo na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Alphayo Kidata.
Mhandisi wa Manispaa ya Kinondoni, Baraka Mkuya alidai wamepewa agizo na Katibu huyo,
kuvunja nyumba ndani ya kiwanja hicho, baada ya kubainika kuwa eneo hilo siyo mali ya Rwakatare, hivyo hastahili kujenga mahali hapo.
Mhandisi Mkuya alidai pamoja kutokuwa mmiliki halali wa
eneo hilo, nyumba hizo pia zimejengwa bila utaratibu, ikiwemo kupata kibali cha
ujenzi kutoka katika manispaa hiyo, suala linaloashiria kuwa kulikuwa na kitu
kimejificha.
“Sisi kama manispaa tumekuja kutekeleza agizo la kubomoa
kutoka kwa Katibu Mkuu, kinachoonyesha ni kuwa aliyejenga eneo hili alivamia
eneo la mtu mwingine huku akijua wazi ni kinyume cha utaratibu” alidai Mkuya.
Alidai matatizo ya uvamizi wa viwanja, yamekuwa ni jambo
la kawaida hasa katika Manispaa ya Kinondoni na kwamba wanaendelea
kuyashughulikia kwa lengo la kuyapatia ufumbuzi wa haraka.
Awali, kazi
hiyo ya ubomoaji ilitanguliwa na ‘vuta nikuvute’ baina ya mwanasheria aliyedai
kuwa anamwakilisha Rwakatare, Emmanumuel Muganyizi na Mhandisi wa Manispaa ya
Kinondoni, Baraka Mkuya kuhusu
suala la kubomolewa kwa nyumba hizo, zinazodaiwa kujengwa ndani ya kipindi
kisichozidi miezi miwili na kupauliwa kwa vigae.
Huku akiwa na nyaraka mbalimbali za kesi, alidai kesi
bado ipo katika Mahakama ya Kinondoni.
Muganyizi alisema anashangazwa na uamuzi huo uliochukuliwa kwa madai kuwa suala hilo, halijapatiwa ufumbuzi wa kisheria na
Mahakama.
“Ninaamini hiki kinachoendelea hapa ni sawa na uvunjifu
wa amani, kesi bado ipo mahakamani inapaswa iachwe iishe ndiyo uamuzi ufanyike.
Kwa hili mnalofanya sasa siyo sawa
kabisa,” alisema Muganyizi.
Mwanasheria huyo wa Rwakatare, awali aliingia katika
mzozo na waandishi, akidai kushangazwa na kitendo chao cha kutaka kuandika
habari hiyo.
Alidai habari hiyo haina manufaa kwa jamii, kwa kuwa
inahusu madai ya mtu na mtu.
Kwa upande wake, mtu anayedai kuwa mmiliki wa kiwanja
hicho, aliyekuwepo wakati kazi ya uboaji ikiendelea, Janeth Kiwia, alidai
kiwanja chake kilivamiwa na kuanza kujengwa mwishoni mwa mwaka jana wakati akiwa safarini kwa watoto wake nje ya
nchi.
Alidai kabla ya kuvamia eneo hilo, kulikuwa na nyumba ya vyumba vinne,
aliyokuwa akiijenga taratibu, ambayo hata hivyo ilibomolewa na msingi wake
kutumika kujenga moja ya nyumba hizo.
“Tayari kulikuwa na nyumba iliyokuwa imefikia usawa wa
rinta, lakini cha kushangaza walipovamia waliibomoa na kujenga ya kwao,
namshukuru Mungu kwa kuwa haki imetendeka baada ya kuhangaika huku na kule
kutafuta haki yangu,” alidai Janeth.
Alidai kitendo hicho, kimemfanya kujenga imani na
Serikali kuwa inatenda haki, bila kujali kuwa aliyekuwa akiporwa na mnyonge,
huku akiitaka kuwasafisha baadhi ya watendaji waliopo ndani ya wizara hiyo,
wanaoshirikiana na watu wabaya kutaka kupora haki za watu.
“Nilikuwa sitarajii kama ningefanikiwa tena kupata
kiwanja changu, namshukuru Mungu haki imetendeka bila hata mimi kutoa Shilingi
moja, naomba tusife moyo na Serikali yetu kwa kuwa inafanya kazi,” alisisitiza
Janeth.
Mwanasheria
aliyekuwa akisimamia kesi ya Janeth, Howard Msechu kutoka Kampuni ya uwakili ya Homac, alidai
mteja wake ndiye mmiliki halali wa kiwanja hicho.
No comments:
Post a Comment