DARAJA LA KIGAMBONI KUKAMILIKA JUNI MWAKANI

Ujenzi wa Daraja la Kigamboni katika Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam umekamilika kwa asilimia 60 na linatarajiwa kuanza kutumika Juni mwakani.
Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli alifanya ziara ya kukagua ujenzi wake na kuridhika na kasi iliyopo huku akitaka watendaji wanaosimamia ujenzi huo, ikiwemo Shirika la Hifadhi za Jamii (NSSF), Wakala wa Barabara (Tanroads) na Wizara ya Ujenzi kuhakikisha linakamilika mwezi huo ili kuweza kufunguliwa na Rais Jakaya Kikwete kabla hajamaliza muda wake.
Magufuli alisema neema kwa wakazi wa Kigamboni, itaanza kabla ya muda huo kwani likikamilika kwa kiwango fulani wataruhusiwa kulitumia na kupunguza usumbufu unaojitokeza kwa kutumia vivuko viwili vilivyopo sasa.
Akizungumza katika ziara yake ya siku moja kukagua ujenzi huo na vivuko viwili vinavyotengenezwa cha Mv Mtwara pamoja na Mv Kigamboni kinachofanyiwa ukarabati wa kawaida, alisema wananchi wa Kigamboni watafurahia usafiri baada ya kukamilika kwa daraja hio.
“Natoa mwito kwa watendaji wote kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilika mwezi Juni mwakani ili Rais Kikwete aweze kufungua mradi huu aliouanzisha, isijetokea mtu mwingine kujitokeza na kujidai na changamoto nyingine zilizopo zitatatuliwa mapema kama wizara ilivyoahidi,” alisema.
Magufuli alisema tayari wamewaondoa watu watano waliokuwa wamekataa kubomoa nyumba zao na kukimbilia mahakamani, ili mradi uweze kuendelea wakati wao wanapambana mahakamani kwani haiwezekani kuzuia mradi wa jamii nzima kwa sababu ya watu watano.
Awali, Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Patrick Mfugale alisema ujenzi huo ulioanza mwaka 2011  kwa kiasi cha Sh bilioni 214.6 na kutarajiwa  kukamilika baada ya  miezi 36 ambayo ni Januari mwakani, umeshindwa kukamilika kutokana na changamoto walizokabiliana nazo.
Alisema changamoto hizo ni katika ujenzi wa chini ya bahari nguzo namba nane kulikuwa na mwanya ambao walipomwaga zege ilikuwa ikipotelea baharini na kusababisha kusitisha ujenzi na kufanya utafiti ambao baada ya kukamilika walimuongezea mkandarasi miezi mitano hadi Julai mwakani.
“Hadi sasa kazi imefikia asilimia 60 na itakamilika Julai mwakani, lakini kutokana na agizo la waziri tunaahidi kukamilisha mwezi Juni mwakani,  jambo ambalo tunaweza ili kuweza kuzinduliwa na Rais Kikwete,” alisema Meneja Mradi kutoka Shirika la NSSF, Karim Mattaka.
Alisema mpaka sasa zaidi ya Sh bilioni 117 zimeshatumika katika ujenzi huo, ambapo Sh bilioni 98 kumlipa mkandarasi, Sh bilioni 11.7 kulipa fidia wananchi ili kupata ardhi ya ujenzi na sh bilioni 7.3 kwa ajili ya malipo ya mhandisi mshauri.
Daraja hilo linalolengwa na serikali kwa ubia baina ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na wakandarasi kutoka China ambao ni China Railways Jiangchang Engineering Co. (T) Ltd na Major Bridge Engineering Co. Ltd.

No comments: