Mkazi wa Kijiji cha Bwekela wilayani Igunga mkoani
Tabora, Kashinje Shima, anatafutwa na Uongozi wa kijiji hicho, kwa kumpa
ujauzito mwanawe wa kumzaa mwenye umri wa miaka 17.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Bwekela, ambaye pia ni Kaimu
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Igoweko, Robert Ruhende, alilaani kitendo
kilichofanywa na mzazi wa mtoto huyo na kusisitiza kuwa sheria lazima ichukue
mkondo wake.
Akisimulia kisa hicho, mke wa mkazi huyo ambaye pia ndiye
mama mzazi wa mtoto huyo, Geni Njiro, alidai alibaini hali hiyo Julai 23 mwaka
huu, baada ya mwanawe wa kiume kumfumania baba yake na dada yake.
Kwa sasa kwa mujibu wa Geni, mwanawe huyo ambaye inadaiwa
amekiri kushiriki kitendo hicho, ana ujauzito wa miezi saba.
Geni alidai kabla ya kugundua kitendo hicho cha kinyama
kilichokuwa kikifanywa na mumewe, alihisi kuwa baba wa mtoto huyo alikuwa
akitumia mwanya wa yeye mama kutokuwepo nyumbani, kufanya vitu visivyo vya
kawaida.
Alidai kuwa alipata hofu kuhusu mwenendo wa mumewe na
mtoto wake siku moja walipokuwa shambani wakiendelea na shughuli za kuvuna
mazao, ambapo mumewe aliaga kurudi
nyumbani.
Kutokana na hofu hiyo, Geni alidai aliamua kumtuma mtoto
wake mkubwa wa kiume, ambaye hakutaka kumtaja jina, akafuatilie nyumbani kupata
uhakika wa kile alichokuwa akihofia.
Mama huyo alidai baada ya mtoto wake huyo kufika nyumbani, ndipo alikuta baba
yake wakifanya ngono na mdogo wake na kurudi shambani na kumpa taarifa mama
yake.
Baada ya taarifa hiyo, mama huyo alidai kuwa aliamua
kuita ndugu wa pande zote mbili, kwa ajili ya kuzungumzia unyama huo, ambapo
baba huyo alipohojiwa katika kikao hicho cha familia, alikana kuhusika na tuhuma hizo.
Hata hivyo, mama huyo alidai babu wa mtoto huyo,
alishauri waende kupima hospitali kupata ukweli, ndipo baba huyo alipokubali
kuwa anatembea na mtoto wake.
Baada ya kukubali, inadaiwa baba huyo alitakiwa kulipa
adhabu ya faini ya ng’ombe wawili, ambao aliwalipa na suala hilo kuwa
limekwisha.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mwina, Bundala Makelema,
alikiri kuwepo kwa suala hilo. Alidai kuwa wakati mtuhumiwa huyo akilipa adhabu
ya kimila ya ng’ombe wawili, yeye alishiriki kwa nafasi yake ya Kiongozi wa
Kitongoji.
Hata hivyo, inadaiwa familia anayotoka mama huyo,
ilipinga uamuzi huo wa kifamilia na kumruhusu ndugu yao, kuchukua hatua zaidi,
ikiwemo kutoa taarifa katika vyombo vya habari.
Taarifa hiyo ilipofika kwa Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha
Bwekela, ambaye pia ni Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kata ya Igoweko, Ruhende ambaye
aliahidi kwenda Polisi ili hatua zaidi zichukuliwe, mama huyo alidai ndipo
mumewe alipoamua kutoroka nyumbani na kwenda kusikojulikana.
No comments:
Post a Comment