INDONESIA, KENYA KUNUNUA MAHINDI NA MPUNGA NCHINI

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, amesema  kilio  cha wakulima kuhusu ukosefu wa masoko ya mazao kitakuwa ni cha  kihistoria muda mfupi ujao baada ya nchi ya Kenya na Indonesia  kueleza kusudio  la kununua  mazao ya chakula  yanayolimwa  kwa wingi  katika mikoa iliyopo  Kanda ya Mashariki.
Bendera aliyasema hayo juzi kabla ya kumkaribisha   mgeni rasmi  Waziri wa  Nchi ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima (Nanenane) kwa Kanda ya Mashariki yaliyofanyika Viwanja  vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,  mjini hapa.
Alisema Kenya kupitia Balozi wake hapa nchini, aliyetembelea maonesho hayo mjini hapa, ameahidi kuwa Serikali ya Kenya imefanya mazungumzo na Tanzania ili  kununua mahindi na mpunga kwa wakulima wa kanda hiyo.
“Uhakika wa kuuza mazao ya wakulima wa Kanda hii ya mashariki umepata majawabu...Serikali ya Kenya, kupitia Balozi wake nchini baada ya kuona maonesho haya ya wakulima na kufurahiwa na uzalishaji wa mahindi na mpunga atarudi ili kuandikiana mkataba wa kununua mahindi na mpunga ukanda huu wa mashariki,” alisema Bendera.
Akiizungumzia Indonesia, alisema pia Balozi wake nchini naye ameahidi nchi yake kununua mazao mengi nchini, ikiwa ni pamoja na mahindi, mpunga, alizeti, ufuta na nyanya.
Hata hivyo, alisema kupatikana kwa masoko ya mazao hayo ni matunda ya kuwepo kwa maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki ambapo kwa mwaka huu yamezaa matunda  baada ya  nchi hizo  kueleza  kusudio  la kununua  mazao ya chakula  yanayolimwa  kwa wingi  katika mikoa iliyopo  Kanda ya Mashariki ambayo ni Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.

No comments: