Watu 135 wameuawa katika
matukio tofauti yaliyotokea mkoani Mbeya katika kipindi cha kuanzia Januari
hadi Julai mwaka huu.
Kiasi hicho
cha matukio ya mauaji ni sawa na pungufu ya matukio 21 sawa na asilimia 14
ikilinganisha na yale 156 yaliyotokea katika kipindi kama hicho mwaka jana.
Akitoa
taarifa ya utendaji wa jeshi la polisi mkoani Mbeya, Kamanda wa polisi mkoani
hapa Ahmed Msangi alisema katika takwimu hizo mauaji yaliyotokana na wananchi
kujichukulia sheria mikononi yalikuwa 33.
Alisema
mauaji yaliyosababishwa na imani za kishirikina yalikuwa 23 sawa na matukio ya
mauaji yaliyotokana na sababu nyingine huku matukio ya mauaji yaliyosababishwa
na wivu au ugoni yalikuwa 20.
Matukio ya
mauaji yaliyotokana na ugomvi wa majumbani yalikuwa 16, matukio ya ugomvi
vilabuni 11 na matukio ya kulipiza kisasi yalikuwa tisa.
Alisema
katika kipindi hicho wahamiaji haramu 159 walikamatwa kati yao 152 walikuwa
raia wa Ethiopia, 23 raia wa Burundi,10 Wasomali, saba Wapakistani, wawili
kutoka Malawi na mmoja akiwa ni raia wa Msumbiji.
“Katika
kipindi hicho tumeweza kukamata bunduki 19 ambapo gobori zilikuwa 15, bastola
mbili zilizotengenezwa kienyeji, Riffle moja na SMG moja. Pia zilikamatwa
silaha mbili baada ya majambazi kuuawa katika jaribio la kufanya unyang’anyi. Silaha
hizo ni SMG yenye namba 3514 na AK-47 namba 592058 na risasi 25 kwenye
magazini,” alisema Kamanda Msangi.
Aliongeza
kuwa katika kipindi hicho kiasi cha lita 479 za gongo pamoja na mitambo 16 ya
kutengenezea pombe hiyo vilikamatwa.
Kilo 296 na
gramu 678 na miche 314 ya bangi zilikamatwa sambamba na mashamba matatu ya
bangi yenye ukubwa wa jumla ya ekari moja na robo.

No comments:
Post a Comment