Sunday, July 13, 2014

RUSHWA YA NG'OMBE, MBUZI YAMKERA KIKWETE

Rais Jakaya Kikwete amewaonya wenyeviti na maofisa watendaji wa vijiji kuacha mara moja tabia ya kupokea rushwa ya mbuzi na ng’ombe kutoka kwa wafugaji wanaohamia kwenye maeneo yao bila kuzingatia taratibu zilizowekwa na vijiji.
Alitoa onyo hilo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Sakura kilichopo wilayani Pangani, ikiwa ni siku ya nne ya ziara yake ya kukagua utekelezaji wa shughuli za maendeleo mkoani Tanga. Alisema vitendo hivyo vinavyoendelea kufanywa na baadhi ya viongozi hao wa vijiji tayari vimeibua migogoro kati ya wakulima na wafugaji, hali inayoendelea kutishia usalama wa wananchi wa maeneo mbalimbali ikiwemo mkoani Tanga.“Nimearifiwa kwamba hapa Pangani watu wanaongezeka kwa kasi …mifugo nayo imeongezeka sana hasa ng’ombe kutoka 21,000 waliokuwepo mwaka 2010 hadi kufikia wastani wa ng’ombe 72,419 mwaka huu …mifugo hali hii kwa hapa kwenu sio nzuri na ninawataka kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya msimamie vizuri kwa kuwa pakitokea migogoro ninyi ndio mtakaoanza kulaumiwa”, alisema na kuongeza: 
“Hili lisimamieni vizuri kwa sababu kule ambako hakuna usimamizi mzuri tayari kumezuka migogoro …Wenyeviti na watendaji wa vijiji acheni kula rushwa kwa kukubali kuhongwa mbuzi na ng’ombe ili kuruhusu wafugaji wa ng'ombe wa kienyeji kuingia vijijini pasipo kuzingatia utaratibu mzuri”. 
Rais Kikwete alisema ili kuzuia migogoro hiyo isiendelee kuibuka kuna haja kwa viongozi kutengeneza utaratibu mzuri wa matumizi bora ya ardhi za vijiji ambao utabainisha mipaka baina ya shughuli za kilimo, ufugaji na nyingine za kijamii.
“Wekeni utaratibu mzuri jamani kwamba kwenye wilaya yetu eneo gani tutafuga na eneo lipi tutalima…acheni kuwachanganya wananchi, unajua uongezekaji wa mifugo usio na utaratibu mzuri unazua migogoro hivyo viongozi jitahidini kulisimamia”, alisema.
Hata hivyo, aliwataka viongozi wa mkoa wa Tanga kuongeza ubunifu wa kuhakikisha wanaongeza msukumo na uhamasishaji wananchi katika ufugaji wa ng’ombe bora wa maziwa badala ya hao wa kienyeji ili kuwezesha uzalishaji endelevu katika Kiwanda cha Maziwa cha Tanga Fresh.“Ufugaji wa kisasa wa ng’ombe wa maziwa nataka uwe mpango wa kila wilaya hapa Tanga, haiwezekani mnacho kiwanda cha Tanga Fresh halafu hakuna maziwa ya kutosha lazima kiwanda hiki mkilishe ili kiwe na uhakika”, alisema.

No comments: