Sunday, July 13, 2014

SHEIN ATAKA UJENZI MKANYAGENI UKAMILIKE

Rais  wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ameiagiza Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuhakikisha shule mpya ya Sekondari ya Mkanyageni inakuwa na mazingira mazuri yanayoizunguka na eneo la kutosha ili kukamilisha ujenzi wake.
Agizo hilo amelitoa juzi wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa shule hiyo inayotarajiwa kuwa ya wilaya iliyopo Mkoa wa Kusini Pemba.Katika maelezo yake kwa Dk Shein, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Abdallah Mzee alisema baadhi ya huduma katika shule hiyo ikiwemo kiwanja cha michezo zitakosekana kutokana na uhaba wa eneo la shule. 
Alifafanua kuwa ingawa eneo hilo ni shamba la Serikali lakini wameshindwa kupewa kwa sababu baadhi ya wananchi wamelichukua na kudai ni lao na wengine tayari wamejenga nyumba za makazi.
Kutokana na maelezo hayo, Dk Shein aliagiza utaratibu ufanyike kuwasiliana na wananchi waliopo katika eneo hilo ili kufahamu kama wapo kisheria au vinginevyo na kusisitiza kuwa taratibu za umiliki wa ardhi lazima zifuatwe.Dk Shein alisisitiza kuwa shule hiyo ambayo ni kati ya miradi mikubwa ya aina yake ya ujenzi wa shule za sekondari Zanzibar ikiwemo ya Kibuteni kisiwani Unguja ujenzi wake lazima ukamilishwe kama ilivyopangwa.Shule za sekondari Mkanyageni na Kibuteni zinajengwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Benki ya Maendeleo ya Uarabuni (BADEA).

No comments: