Sunday, July 13, 2014

SHILINGI BILIONI 3 ZATENGWA KUNUNUA KIVUKO PANGANI

Serikali imetenga kiasi cha Sh bilioni tatu katika bajeti ya mwaka huu wa fedha kwa ajili ya kununua kivuko cha pili cha Mv Pangani.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Rais Kikwete alipohutubia wakazi wa kijiji cha Bweni wilayani Pangani baada ya kuzindua mradi wa majisafi kijijini hapo.Alisema lengo la ununuzi wa kivuko hicho ni kuendelea kuboresha huduma ya usafirishaji kwa kurahisisha ufanisi wa shughuli za uchukuzi na kiuchumi wilayani humo.“Tumeona kuna umuhimu mkubwa wa kuongeza kivuko cha pili hapa kwenye mto Pangani ili kurahisisha shughuli za uchukuzi, lakini pamoja na vivuko hivyo napenda kuwaahidi kwamba baadaye utakapokamilika ujenzi wa barabara ya lami hapa ni dhahiri shughuli za uchukuzi zitaongezeka,” alisema na kuongeza:“Wakati huo ukifika serikali inao mpango wa kuongeza kivuko kingine kikubwa zaidi ambacho kitakuwa na uwezo wa kuingia magari kati ya 60 hadi 70 pamoja na kuchukua watu 200 kwa wakati mmoja”. 
Akizungumzia ujenzi wa barabara kuu ya Tanga- Pangani, Saadani- Bagamoyo alisema serikali imeendelea kuchukua hatua thabiti kuishughulikia ambapo sasa fedha za ujenzi zinatafutwa.
“Katika barabara hii tayari hatua tatu muhimu zimekamilika ikiwemo ile ya upembuzi yakinifu, tathmini ya ubora wa kiuchumi nayo ilishakamilika pamoja na usanifu na sasa tunatafuta fedha,” alisema. 
Rais Kikwete aliongeza, “Sasa tunaendeleza jitihada za kupata fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi huu wa ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami na tunashukuru kwamba mambo sio mabaya”.
Hata hivyo, kuhusu ujenzi wa barabara za lami ndani ya wilaya hiyo alibainisha kwamba katika bajeti hii serikali pia imetenga kiasi cha Sh milioni 519 ili kuzifanyia matengenezo barabara hizo.

No comments: