Sunday, July 13, 2014

MALIASILI MPANDA WAKUSANYA SHILINGI MILIONI 260

Idara  ya  Ardhi, Maliasili  na Mazingira  katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda  imekusanya zaidi Sh milioni 260 katika kipindi  cha  mwaka mmoja  kilichoanzia Julai   mwaka jana hadi Juni  mwaka huu.
Hayo yalielezwa  juzi  na Kaimu  Ofisa Ardhi,  Maliasili  na  Mazingira  wa halmashauri hiyo,  Josephina Rupia  wakati akisoma  taarifa ya utekelezaji  wa  shughuli  za idara hiyo   kwa kipindi  cha mwaka  2013 na 2014  katika kikao cha Baraza la Madiwani  kilichoketi mjini hapa. Alisema idara hiyo ilikusanya  kiasi cha Sh  265,290,050 kama mapato ya ndani. Alisema  Sh 260,780, 000  zilitokana  na  ushuru  wa leseni za mbao na Sh 210,750 ilikuwa ni makusanyo  ya  ushuru wa magobole.
Alisema Sh 296,500 ni  ushuru wa asali na kuingia porini, Sh 914,000 zilikuwa ni ada ya fomu za viwanja  na Sh  3,868,800 zilitokana na  ushuru wa  uwindaji wa kienyeji.
Alisema  katika  kipindi  hicho  cha mwaka mmoja  idara hiyo  imeweza kufanya  doria mbili kubwa  na kufanikiwa  kukamata  mbao  na magogo yaliyovunwa bila kibali  pamoja na magunia  369 ya mkaa na wanashikilia baiskeli  tisa  ambazo wavunaji haramu wa maliasili walikimbia na kuzitelekeza. 
Pia idara hiyo  ilikamata  ng’ombe 280 ambao  walikuwa wameingizwa  katika msitu wa Hifadhi  wa  Nkaba  kinyume cha  sheria  ambapo  wamiliki watatu  wa mifugo hiyo wamekamatwa na kufikishwa mahakamani.
Rupia alilieleza  baraza hilo lililokuwa likiongozwa na Mwenyekiti  wake, Yassin Kibiriti  kwamba  idara hiyo ilifanya  operesheni  ya  kuondoa  makazi holela  na watu 361 wameondolewa kwa nguvu  na kati yao 15  wamefikishwa mahakamani.

No comments: