MWANAFUNZI BORA MASOMO YA SAYANSI AFICHUA SIRI YAKE

Mmoja wa wanafunzi waliofanya vizuri kitaifa katika masomo ya Sayansi, Isaack Shayo ameweka wazi mbinu alizozitumia  kufanikisha ufaulu wake .
Akizungumza na gazeti hili  jana nyumbani kwao jijini Dar es Salaam, Isaack  (20) ambaye alihitimu Shule ya Sekondari ya St Joseph’s Cathedral  alisema, pamoja na mbinu nyingine, aliwasumbua walimu kutafuta maarifa na pia alihangaika kujitafutia vitabu.
Isaack yumo kwenye kundi la watahiniwa 10 bora kitaifa kwa masomo ya Sayansi na pia kwenye kundi la wavulana bora kitaifa katika masomo hayo.
Kijana huyo ambaye alikuwa akichukua masomo ya Fizikia, Kemia na  Hisabatu (PCM), alisema aliamini anaweza kufaulu lakini hakufahamu ni kwa alama zipi.
Katika matokeo yaliyotangazwa jana, amepata alama 4. Fizikia amepata B+, Kemia A, Hisabati A pamoja na  Sayansi ya Kompyuta (somo la ziada) amepata A.
Alisema chanzo cha yeye kupata ufaulu huo ni kujituma katika kusoma na pia kutafuta vitabu mbalimbali na pia kusumbua walimu alipoona amekwama.
"Nimefurahi sana lakini pia mbali na kufanya hayo yote pia kumwomba Mungu na kusali sana pia naamini kumenisaidia kuweza kupata matokeo haya mazuri," alisema Isaack.
Isaack  alisema  pia walimu waliomfundisha wamechangia kutokana na ufundishaji mzuri.
Alisema ndoto yake ni kuwa Mhandisi wa Ujenzi na anaamini atafanikiwa.
Akizungumzia  changamoto alizokumbana nazo katika kusoma, alisema miongoni ni kutokuwepo vitabu vya Kidato cha Tano na Sita vya hapa nchini. Kwa mujibu wake, alilazimika kujisomea vitabu mbalimbali alivyoona vinahusu masomo anayochukua vikiwemo vya nje ya nchi
“Lakini nilijitahidi sana kusoma vitabu vingi ambavyo vipo pale kwenye maktaba ya shule kwa kuhakikisha nakuwa napata kile ninachokitaka," aliongeza Isaack.
Alisema hakuna jambo la ziada zaidi ya kusoma, kuwasumbua walimu na kusali yaliyomfanya afanye vizuri.
Kijana huyo anashauri wanafunzi wengine kuhakikisha wanafuata mambo hayo ambayo yanaweza kuwapa matokeo mazuri katika masomo yao.
Kwa upande wake, mama mzazi wa Isaack, Jane Mgaya alisema,  mtoto huyo ni mtulivu na mwelewa.
Kwa mujibu wa mama huyo ambaye ni Katibu Muhtasi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, hata wakati mtoto wake akiwa Darasa la Saba katika Shule ya Msingi Filbert Bayi, aliongoza kwa kuwa mwanafunzi bora.
“Hata alipokuwa Kidato cha Nne pia alifaulu vizuri kwa kupata daraja la kwanza. lakini jambo lingine alikuwa ni mtundu sana unaweza ukamnunulia mdoli wa ndege lakini ukakuta amefungua yote. Unagombana naye kwa kudhani ameharibu lakini baadaye anarudisha kama ilivyo," alisema Jane.

No comments: