MKATABA WA GESI STATOIL NA SERIKALI HADHARANI

Serikali imeondoa utata unaohusu mkataba wa gesi wa nyongeza baina yake na kampuni ya Norway ya Statoil, kwa kuanika wazi mgawanyo unaoonesha Tanzania itapata faida kubwa ya asilimia 61 wakati kampuni hiyo itapata asilimia 39.
Mgawanyo huo unatokana na makubaliano yaliyofikiwa baina ya kampuni hiyo na Serikali baada ya makubaliano ya kwanza kupitia mkataba wa mafuta kutotekelezeka kutokana na kampuni hiyo kugundua katika bahari yenye kina kirefu, kiasi cha 42.5 futi za ujazo za gesi asilia badala ya mafuta katika utafiti wake.
Hayo yalibainishwa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Yona Kilagane, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utata huo, uliobainishwa na baadhi ya vyombo vya habari, ikiwemo mitandao ya kijamii.
Kauli ya shirika hilo, inakuja siku kadhaa baada ya kuenea katika mitandao hiyo na baadhi ya vyombo vya habari taarifa kuwa, mkataba huo wa nyongeza baina ya Serikali na kampuni hiyo, umelenga kuinufaisha zaidi kampuni ya Statoil huku Tanzania ikitarajiwa kupata hasara ya Sh trilioni 16 kila mwaka.
Akitoa ufafanuzi kuhusu suala hilo, Kilagane alisema taarifa hizo hazina ukweli wowote kwa kuwa kupitia mkataba huo wa nyongeza, Tanzania ndio itakayonufaika zaidi kuliko kampuni hiyo tofauti na inavyodaiwa.
"Nafikiri kilichotokea ni kushindwa kuuelewa na kuutafsiri mkataba, kampuni hii tumeingia nayo mkataba wa mafuta tangu mwaka 2007 kwa ajili ya kutafuta mafuta chini ya mfumo wa mgawanyo wa mapato (PSA), lakini kupitia visima vyake tisa, iligundua gesi katika visima vinane na kimoja kikiwa kikavu," alisema Kilagane.
Alisema awali wakitangaza zabuni kwa ajili ya utafiti wa mafuta hayo, Serikali ilitoa vigezo vya sifa ya kampuni inayotakiwa, ikiwemo kuwa na uwezo kifedha, kuzingatia maslahi ya Watanzania lakini pia ikubali mgawo endapo mafuta hayo yatapatikana uwe wa asilimia 50 kwa 50.
Alisema katika zabuni hiyo, Serikali ilitoa vitalu vinane kwa ajili ya kufanyiwa utafiti wa gesi na kupokea maombi kutoka kampuni tatu ikiwemo hiyo ya Statoil, ambayo baada ya majadiliano ilipatiwa kitalu namba mbili kilichokuwa na visima tisa.
“Hata hivyo, kampuni hiyo ya Statoil mapendekezo yake yalitaka mgawanyo uwe Serikali asilimia tano na wao asilimia 95, jambo ambalo halikukubaliwa na kupitia majadiliano, kampuni hiyo ikaridhia mgawanyo uwe Serikali asilimia 56 pamoja na TPDC na kampuni hiyo ipate asilimia 44,” alisema.
Alisema sababu za kampuni hiyo kutaka kiwango hicho ni kutokana na gharama kubwa za utafiti huo ambao ulikuwa ukifanyika katika kina kirefu cha bahari na kwamba gharama zote katika utafiti huo ni za kubahatisha kwa kuwa endapo mafuta hayo hayatopatikana itapata hasara.
Alisema kwa mujibu wa mkataba wa mafuta, kipo kipengele kinachobainisha uwezekano wa kupatikana gesi badala ya mafuta, ambacho kimefafanua kuwa endapo hilo litatokea, pande zote mbili yaani kampuni hiyo na Serikali lazima zikutane na kukubaliana namna ya kugawana rasilimali hiyo.
Alisema katika utafiti wake ambao ulitumia takribani Dola za Marekani bilioni 1.5, kampuni hiyo ya Norway iligundua gesi badala ya mafuta hali iliyosababisha pande hizo mbili kukutana mwaka 2012 na kukubaliana namna ya kugawana rasilimali hiyo kwa faida ya pande zote.
“Kwa mujibu wa makubaliano Serikali imepata zaidi kwa sababu pia tumegundua fursa zaidi ya kupata gesi na hata Shirika la Fedha Duniani (IMF) limethibitisha hilo wakati lilipokokotoa mgawanyo huo ambapo lilibainisha kuwa Tanzania itapata asilimia 84 dhidi ya kampuni hiyo ya Norway,” alisema.
Akizungumzia mkakati wa Serikali baada ya kugundulika kwa gesi hiyo na Statoil, inatarajia kuweka mtambo wa kusindika gesi hiyo kwa ajili ya kuuza nje ya nchi lakini kipaumbele kikiwa matumizi ya gesi hiyo nchini ambapo TPDC itatengewa eneo kwa ajili ya viwanda hapa nchini.
Hadi sasa jumla ya trilioni 50.5 za ujazo za gesi zimegunduliwa nchini ambazo ni sawa na mapipa bilioni 9.6 zaidi ya Uganda ambayo imegundua mapipa ya gesi kati ya milioni tatu hadi nne. Kati ya gesi hiyo trilioni 42.5 iligunduliwa kwenye kina kirefu cha bahari na trilioni iligunduliwa nchi kavu.
Tanzania ina mikataba 27 na kampuni 18 zinazoshughulika na utafiti wa mafuta, ambazo zimechimba visima 80 kati ya hivyo 30 vimegunduliwa kuwa na gesi sawa na asilimia 40.

No comments: