KAIRUKI ATAKA MAELEKEZO YA MAHAKAMA YATEKELEZWE

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angellah Kairuki amesema ipo haja ya kuwepo kwa usajili wa ufuatiliaji wa matunzo ya watoto ili kwamba maelekezo yanayotolewa na mahakama yaweze kutekelezwa kama inavyostahili.
Aidha, ameyataka mashirika yanayotoa huduma ya msaada wa sheria kwa jamii kuona namna ya kuwapata wanaume wa mfano watakaokuwa vinara wa kuelimisha namna ya kupinga ukatili wa kijinsia.
Alisema hayo jana Dar es Salaam kwa nyakati tofauti katika ziara yake aliyoifanya katika Chama cha Msaada wa Kisheria kwa Wanawake Tanzania (TAWLA) na Kituo cha kutetea haki za wanawake na watoto (TWCWC).
Akiwa TWCWC, Angellah alisema atafuatilia kwa wanaohusika kuhusu kuwepo kwa usajili wa matunzo ya watoto, lengo likiwa ni kuwakomboa wale wanaoathirika.
“Nimesikiliza kwa makini maelezo yatolewayo na waathirika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia…naona ipo haja ya kuwepo kwa rejesta hiyo ili kwamba maelekezo yote yanayotolewa na mahakama kuona kama yanatekelezwa kama ipasavyo,” alisema Angellah.
Aliongeza kuwa ni wakati sasa kwa viongozi  mbalimbali wakiwemo wa dini na hata wa kata kuhakikisha wanatoa elimu katika jamii kuhusu namna ambavyo wanaoathirika na vitendo mbalimbali kuweza kutafuta haki zao na kuzipata.
Aliwataka wale wanaotoa msaada wa kisheria kwa wananchi wakiratibiwa na mashirika hayo kuwa waadilifu na kujikita katika miongozo ya kazi na tabia na mwenendo wao uwe safi ili kuweza kuendelea kujenga imani kwa wanaowahudumia.
Kuhusu kuwepo kwa wanaume wa mfano wa kuelimisha kuhusu ukatili, aliyataka mashirika hayo kuangalia ni namna gani ambavyo watafanya kazi na wanaume ili kwamba katika mikoa ya pembezoni kuweza kuwapata watakaoweza kuwa vinara wa kupinga ukatili wa kijinsia.
Awali Wakili kutoka TWCWC, Gloria Misana alisema mawakili wanaokuwa wakiwatetea wananchi wasiokuwa na uwezo hukabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo ucheleweshaji wa kesi jambo ambalo baadhi ya wateja wao hufikia hatua ya kukata tamaa na kushindwa kuendelea kufuatilia.
Alisema pia utekelezwaji wa hukumu ni tatizo pia kwa vituo vya sheria ambapo wakati mwingine mteja wao hufikia hatua ya kushindwa kupata mali kama ambavyo mahakama inakuwa imeamuru.
Naye Mkurugenzi Mtendaji TAWLA, Tike Mwambipile alisema kutokana na kuongezeka kwa matukio mengi ya ukatili wa kijinsia, wanaona ni muhimu kuwa na nyumba kwa ajili ya kuwapumzisha wanawake wanaokuwa wameathirika na vitendo hivyo.
Alisema lengo sio kuwasambaratisha kutoka kwa waume zao badala yake ni kufanya kila jitihada za kuwaunganisha, kuwaimarisha kiuchumi pamoja na kujua haki zao pamoja na watoto wao.

No comments: