WATANZANIA KUPELEKWA CANADA KUJIFUNZA GESI NA MAFUTA

Serikali ya  Tanzania inatarajia kutuma wataalamu kwenda Canada katika Kamisheni ya Mafuta na  Gesi ya jimbo la British Columbia (BC Oil& Gas Commission), kujifunza udhibiti wa mafuta na gesi.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati, Charles Kitwanga wakati akizungumza na watendaji wa Kamisheni ya Mafuta na Gesi ya Jimbo la British Columbia katika ofisi za kamisheni hiyo zilizo katika mji wa Victoria nchini Canada.
Akiongoza ujumbe wa Tanzania uliotembelea Kamisheni hiyo ili kujifunza masuala ya udhibiti wa sekta ndogo ya gesiasilia na mafuta, Naibu Waziri alisema kuwa lengo la serikali ya Tanzania ni  kuhakikisha kuwa rasilimali zilizopo zinaendelezwa na faida yake kuonekana kwa wananchi, ndio maana wanapanga kuwatuma wataalamu wake kujifunza masuala hayo nchiniCanada .
Naye Ofisa Mkuu wa Operesheni katika Kamisheni hiyo, Ken Paulson alieleza kuwa taasisi hiyo ambayo imeanzishwa miaka 15 iliyopita ina jukumu la kudhibiti shughuli zote za mafuta na gesiasilia ikihusisha, utafiti, uendelezaji na usafirishaji wa rasilimali hizo kwa njia ya bomba.
Paulson alieleza kuwa kamisheni hiyo pia ina jukumu la kukusanya takwimu za kijiolojia zinazotumika katika shughuli za utafutaji wa gesiasilia na mafuta na kuzitangaza kwa njia ya zabuni ili kampuni zinazohitaji kufanya shughuli za utafutaji mafuta na gesi katika jimbo hilo zinunue takwimu hizo kutoka Kamisheni hiyo.
"Ingawa tunasafirisha gesi kwenda Amerika Kaskazini,  mahitaji ya soko hilo yanashuka kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa gesi nchini Amerika, hata hivyo tumejipanga kukabiliana na hali hiyo kwa kutumia gesi hii kwa masuala mengine ikiwemo kuzalisha methano, matumizi ya majumbani na kutumika katika vivuko ambavyo vitakuwa vinatumia mafuta na gesi," alisema Paulson.
Kuhusu mfumo wa ugawanaji mapato (PSA) kati ya makampuni ya utafutaji na uchimbaji gesiasilia na mafuta, Paulson alieleza kuwa kampuni ikianza uzalishaji wa gesi au mafuta, serikali ya jimbo hilo hukusanya mrabaha wa asilimia 10 hadi 20 ya mapato.
Katika ziara hiyo ya mafunzo nchini Canada, Naibu Waziri Nishati na Madini ameambatana na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Victor Mwambalaswa pamoja na baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo akiwemo, Murtaza Mangungu, Raya Ibrahim, Richard Ndasa, Deogratias Ntukamazina, Shafin Sumar na wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na Madini.

No comments: