Mchakato wa usaili kwa
ajili ya kujaza nafasi za Mkaguzi Msaidizi wa Uhamiaji zinazohitajika,
unaendelea licha ya waombaji 4,834 kuchujwa katika awamu ya kwanza.
Kati ya waombaji 6,116
waliofanyiwa usaili hivi karibuni jijini Dar es Salaam, waombaji 1,281 ndiyo
wamebaki wakisubiri duru ya mwisho ya usaili, wabaki 70 watakaojaza
nafasi hizo.
Taarifa iliyotolewa na
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Isaac Nantanga,
ilisema awali waombaji 10,801 waliitwa kwa ajili ya usaili wa kwanza baada kupokea
maombi yao ingawa waliohudhuria walikuwa 6,115.
Alisema hatua hiyo
iliwezesha kupatikana kwa kundi litakalofanyiwa usaili mwingine Juni 23 hadi
Julai 3, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Msemaji
huyo wa Wizara, katika awamu ya pili, usaili utakuwa wa maswali ya ana kwa ana
ukilenga kupima uwezo wa msailiwa kujieleza na kufafanua mambo.
Alisema usaili wa
kwanza, ulikuwa wa kuandika na ulihusisha maswali ya hesabu na ufahamu wa
jumla.
Kuchaguliwa kwa wasailiwa
hawa kulifanyika baada ya kusahihisha majibu yao na majina kuingizwa katika
mfumo wa kimtandao ambao ulisaidia kuchagua wasailiwa waliopata alama 50 na
kuendelea.
Taarifa ya Wizara imeweka
majina ya wasailiwa katika tovuti yake; www.moha.go.tz na ya Idara ya
Uhamiaji, www.uhamiaji.go.tz.
Wasailiwa wote wanatakiwa
kwenda na vyeti vyao halisi vya kuzaliwa, vya shule na picha mbili za pasipoti.
Usaili wa awamu ya kwanza
uliofanyika Dar es Salaam hivi karibuni, uligeuka gumzo kutokana na idadi kubwa
ya watu walioitwa, jambo ambalo halijawahi kushuhudiwa.

No comments:
Post a Comment