Mjadala wa Bajeti Kuu ya
Serikali umeendelea kushika kasi bungeni mjini hapa ambapo wabunge wameitaka
Serikali kuwa makini na mashambulizi ya kigaidi yanayotokea nchini Kenya
kwa vile yanaweza kuathiri sekta ya utalii nchini.
Mbali ya onyo hilo
wabunge pia wameitaka Serikali kuangalia uwezekano wa kuwatoza kodi wamiliki wa
nyumba za kupanga, kama chanzo kipya cha kuongeza mapato yake.
Akichangia kwenye mjadala
huo jana, Mbunge wa Viti Maalumu, Cynthia Ngoye (CCM), alisema
mashambulizi ya kigaidi yanayofanyika nchini Kenya, yataathiri sekta ya
utalii nchini.
Mbunge huyo alisema
takwimu zinaonesha kuwa asilimia 40 ya watalii huingia nchini kupitia mpaka wa
Namanga, hatua inayodhihirisha kuwa wapo watalii ambao huingia nchini wakitokea
Kenya.
Ngoye alisema kwa sasa
badhi ya watalii waliokuwa waje nchini, wameshaanza kusitisha safari zao
kutokana na mashambulizi hayo.
Kutokana na hali hiyo,
Mbunge huyo alitaka Serikali kuwa makini katika hatua zozote za kuongeza kodi
katika sekta ya utalii.
Kuhusu kuongeza wigo wa
mapato, Ngoye alitaka Serikali kuangalia uwezekano wa kutoza kodi wamiliki wa
nyumba za kupanga, kiwe chanzo kipya cha mapato.
“Mheshimiwa Spika wakati umefika sasa kwa
wamiliki wa nyumba za kupanga kutozwa kodi. Tukikitumia chanzo hiki vizuri
Serikali itaweza kupata fedha nyingi na kujiongezea mapato,” alisema.
Kwa upande wake Mbunge wa
Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF), alieleza kushangaa sababu za Serikali
kutotaka kuchukua mapato kutoka katika sekta ya uvuvi katika bahari kuu.
Alisema Serikali iliwahi
kufanya utafiti na kubaini karibu dola za Marekani milioni 222 zimekuwa
zikipotea kila mwaka, kutokana na kukosekana kwa udhibiti wa uvuvi katika
bahari kuu.
Hata hivyo, katika
utafiti huo, Hamad alisema Serikali ilieleza imekuwa haipati mapato kutoka
katika uvuvi wa bahari kuu kwa kuwa haina bandari ya meli za uvuvi, na kama
wakiamua kuanza kutoza kodi, kuna uwezekano wa wawekezaji kuondoka, sababu
alizosema si za kweli.
Alisema inashangaza kuona
kuwa wakati Serikali ikihangaika kupata mapato yatokanayo na leseni katika meli
chache za uvuvi, zipo meli zaidi ya 360, zinavua katika bahari kuu mamia
ya tani za samaki bila kibali.
Kwa mujibu wa Hamad,
wataalamu wa Serikali waliwahi kushauri kufanyike mnada wa kimataifa, ili
wavuvi waje na malengo yao na Serikali iwapangie tozo zake ili kupata mapato
stahiki lakini, ushauri huo haukuwahi kufanyiwa kazi.
Mbunge huyo pia aliitaka
Serikali kuwa makini na uendelevu wa sera na miradi yake, akitolea mfano wa
mipango na sera za Serikali katika kilimo.
Alisema bajeti ijayo ya
2014/2015, inaonesha kuwa kipaumbele kikubwa ni elimu, hivyo akataka Serikali
kueleza inatarajia kupata wanasayansi wangapi na katika muda gani na
wahandisi wangapi.
Kwa upande wake Mbunge wa
Kawe Halima Mdee (Chadema) akichangia jana alisema kazi ya upinzani si kusifu
Serikali, bali ni kukosoa utendaji wa Serikali na idara zake zote na kazi ya
pili ni kutoa mawazo mbadala.
Alisema hata punguzo la
kodi ya mshahara (PAYE), kwa wafanyakazi kutoka asilimia 13 katika mwaka unaoisha
wa fedha, mpaka asilimia 12 katika mwaka ujao wa fedha limetokana na shinikizo
kutoka Kambi Rasmi ya Upinzani, akidai ilikuwa ni hoja yao ya siku
nyingi.
Akichangia juzi
jioni Mbunge wa Viti Maalumu, Leticia Nyerere (Chadema) aliwataka wabunge
wenzake wakiwemo wa Kambi Rasmi ya Upinzani, wanapoikosoa Serikali kwa
kutokusanya kodi vizuri, wajiulize kama nao wanalipa kodi.
Nyerere aliisifu Serikali
kwa kutoa huduma za kijamii zikiwemo za maji katika Jimbo la Kwimba, Mwanza
anakotoka na kufafanua kuwa, anaposema ukweli kuhusu mambo yaliyofanywa na
Serikali, kuna baadhi ya wenzake wa upinzani hawafurahi.

No comments:
Post a Comment