Bodi ya Wakurugenzi wa
Benki ya Dunia, imeidhinisha msaada kwa Tanzania zaidi ya Sh bilioni 74
kusaidia upatikanaji wa huduma ya maji safi, salama na maji taka kwa familia
masikini za mijini na vijijini.
Fedha hizo sawa na Dola
za Marekani milioni 44.9 ziliidhinishwa kama mkopo ikiwa ni fedha
za ziada za kuboresha Mradi wa Kusaidia Sekta ya Maji (WSSP).
Mradi wa WSSP
uliidhinishwa na Bodi mwaka 2007, na umechangia awamu ya kwanza ya Programu ya
Maendeleo ya Sekta ya Maji Tanzania (WSDP) wa miaka 20 kuanzia mwaka 2006 hadi
2025.
Mradi huo unaendeshwa na
Serikali, wadau wa maendeleo na wadau wengine na tayari umekuwa na matokeo
chanya, kama vile ukamilishwaji wa miradi ya maji katika vijiji 918.
Miradi mingine ni pamoja
na ujenzi na ukarabati wa vituo vya maji 26,468 inayolenga kunufaisha wananchi
milioni 6.7 wa vijijini, kusaidia upatikanaji wa huduma ya maji kwa wakazi
milioni 2.8 wa mijini na kusaidia serikali za mitaa kwa ajili ya kuboresha
mfumo wa maji taka kwa kaya 180,000.
"WSSP inatoa fursa
sawa ya huduma ya maji safi na maji taka, ambayo ni mambo muhimu kwa afya bora
na kuboresha maisha ya jamii masikini za mijini na vijijini nchini
Tanzania," alisema Mkurugenzi Mwakilishi wa Benki ya Dunia Tanzania
Philippe Dongier kupitia taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari.
Chini ya mradi huo wa
WSSP, uboreshaji wa huduma ya maji utahusu ujenzi wa vituo
vya maji katika vijiji 628 ukilenga kunufaisha watu 234,624.
"Kwa kuleta huduma
za maji kwa jamii masikini katika vijiji na maeneo ya mijini, WSDP itawezesha
wasichana na wanawake kutumia muda kidogo kuchota maji kwa ajili ya familia zao
na muda mwingi kwenye elimu na shughuli za kiuchumi," alisema kiongozi wa
mradi kutoka Benki ya Dunia, Yitbarek Tessema.
Hivi karibuni, Bunge
lilidhinisha Sh 520,906,475,000 kwa ajili ya Wizara ya Maji, na asilimia 94 ya
fedha hizo zitatumika kwenye miradi ya maendeleo zikiwamo Sh bilioni saba
zilizotengwa kwa ajili ya kulipa fidia wananchi ili kupisha mradi wa Bwawa la
Kidunda litakalotumiwa kukabili adha ya maji jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment