Shirika la Madini la
Taifa(Stamico), limetangaza kujisuka upya na kutangaza rasmi neema kwa
wachimbaji wadogo wa madini.
Chini ya mkakati huo wa
kuhakikisha linajiendesha kwa faida, wachimbaji wadogo watawezeshwa
mashine za kisasa za uchimbaji na kuhakikisha wazawa pia
wanawekeza kwenye rasilimali za taifa kwa faida.
Kadhalika, mkakati
mwingine ni kuhakikisha shirika hilo linajiendesha kwa faida na kupeleka fedha
Hazina, badala ya kutegemea Serikali kuliendesha.
Akizungumza na waandishi
wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Stamico,
Mhandisi, Edwin Ngonyani alisema hizo ni kazi mbili muhimu anazotaka kuzifanya
ndani ya shirika hilo na kuhakikisha linajiendesha lenyewe bila utegemezi
wa Serikali kuanzia miaka miwili ijayo.
“Nimeanza kazi rasmi hapa
Juni mosi mwaka huu, kazi zangu kuu ni mbili na ndizo nitakazohakikisha
zinatekelezwa, moja ni kurekebisha shirika, liwe linapeleka fedha Hazina, hii
tabia ya mashirika ya Serikali ya kuchukua fedha Hazina itakoma kwa
shirika hili, na mbili ni kuwasaidia wachimbaji wadogo wa madini,” alisema
Ngonyani.
Alisema kwa miaka miwili
kuanzia sasa, shirika hilo litaomba kuwezeshwa fedha na Serikali kama
mtaji na baada ya hapo litajiendesha na litapeleka fedha
Hazina na hiyo inawezekana kupitia miradi yake mingi iliyoanza na mingine
itakayoanza uzalishaji hivi karibuni.
Akizungumzia mkakati kwa
wachimbaji wadogo, Ngonyani alisema, ndani ya miaka miwili ijayo, shirika hilo
litanunua mitambo miwili ya uchimbaji wa kisasa ambayo wataitumia na kwa
kuanzia, gharama za ulipiaji mitambo hiyo, shirika litaitoza Serikali.
Alisema baada ya muda,
wachimbaji hao watazoeshwa na kueleweshwa umuhimu wa kuchangia gharama na kisha
baadaye watatozwa gharama hizo baada ya wao kuanza kufaidika na uchimbaji wa
kisasa.
“Tunataka wachimbaji
wadogo wa madini nchini wanufaike na wao wawe sehemu ya uwekezaji kwenye
rasilimali zao, kama ambavyo hao wawekezaji wa nje wanavyowekeza, na sasa
Watanzania nao watawekeza, kwani hao wametoa fedha zao mfukoni za mtaji? Si
benki zimewakopesha na sisi watu wetu watakopeshwa na benki, ila lazima
tuwawezeshe,” alisema Ngonyani.
Alisema lengo la Stamico
kwa wachimbaji wadogo ni kuhakikisha wanawezeshwa kuwekeza na kuchimba kisasa
ili pia watoa mitaji ambao ni benki, wawe na uhakika wa fedha zao kurejeshwa.
Kwa mujibu wa mtendaji
huyo, ikibidi, shirika hilo litawawekea dhamana wachimbaji wadogo
wawezeshwe kibenki.
Alisema hilo litawezekana
baada ya mkakati wao wa kuanzisha na kuboresha taarifa za wachimbaji wadogo zikiainisha
mahali walipo, aina ya madini wanayochimba na mahitaji yao.
Mkakati mwingine ni
kubaini vyanzo vya migogoro kwenye maeneo ya wachimbaji na kutafuta suluhu
ikiwa ni pamoja na kutenga maeneo yanayofaa kwa uchimbaji mdogo kuepusha
migogoro isiyo ya lazima.
Katika hatua nyingine,
Ngonyani alizungumzia mradi wa uchimbaji madini kwenye mgodi wa dhahabu wa
Tulawaka ambao hivi sasa umenunuliwa na shirika hilo na kuitwa Biharamulo
unaosimamiwa na kampuni ya Stami Gold.
Alisema mgodi huo utaanza
kazi rasmi Agosti 8, mwaka huu na kwamba baada ya miaka miwili na nusu,
watapata faida ya Sh bilioni saba.
Awali mgodi huo ulikuwa
ukimilikiwa na Kampuni ya Barrick Gold na mwishoni mwa mwaka jana, Stamico
ikaununua kwa dola milioni tano.
Kuuzwa kwa mgodi huo
kutoka Barrick kwenda Stamico, kunatajwa kulitokana na mwekezaji huyo wa
awali kuona gharama za uendeshaji ni kubwa hivyo akaamua kuacha uwekezaji.
Kwa upande wake, Meneja
Uchorongaji wa Stamico, Alex Rutagweleka alisema hivi sasa miradi mitano iko
kwenye ubia na shirika hilo kwa ajili ya uwekezaji.
Miradi hiyo ni pamoja
na mgodi wa dhahabu wa Itetemia ambao Stamico imeingia ubia na
Kampuni ya Madini ya Tancan Ltd.
Mradi mwingine ni wa
Buckreef ambao ni wa dhahabu ulioko Geita. Pia Stamico imeingia ubia na
Kampuni tanzu ya Tanzam 2000, ambapo Stamico wana hisa asilimia 45 na 55 iko
kwa kampuni hiyo na kwamba wanategemea uzajishaji utaanza Novemba mwaka huu.
Vile vile upo mradi wa
Kiwira unaozalisha makaa ya mawe kwa ajili ya kufua umeme utakaounganishwa
kwenye gridi ya Taifa.
Kwa mujibu wa Meneja
Fedha na Utawala wa Stamico, Peter Gembe, hivi sasa mradi huo ni wa ubia na
Kampuni ya JV Partnership. Lengo ni kufua megawati 200 za umeme kwa ajili ya
kuunganisha kwenye Gridi ya Taifa.
“Tunapanua mgodi chini ya
ardhi, awali mgodi ulikuwa unazalisha tani 150,000 za makaa ya mawe ila sasa
tunataka zifike tani 300,000, pia tutajenga mitambo mipya ili iwe na uwezo wa
kuzalisha hizo megawati 200 badala ya zile sita za awali,” alisema Gembe.
Stamico ni Shirika la
Umma lililoanzishwa mwaka 1972 kwa lengo la kuongeza mchango wa sekta ya madini
katika pato la Taifa na kuzalisha nafasi za ajira kwa Watanzania.

No comments:
Post a Comment