Ikiwa
zimebaki siku 10 kufungwa kwa shughuli ya kupokea maombi ya mikopo ya elimu ya
juu kwa mwaka wa masomo 2014/2015, takribani wanafunzi 39,000 wameshatuma
maombi yao kwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).
Akizungumza
jana kwenye maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika kwenye viwanja
vya Mnazi Mmoja, Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano (HESLB), Cosmas
Mwaisobwa alisema idadi hiyo ni kwa wanafunzi wapya pekee.
HESLB
ilifungua dirisha la kutuma maombi ya mikopo kwa mwaka wa masomo 2014, Aprili
mwaka huu na maombi hayo yamekuwa yakifanywa kwa njia ya mtandao (OLAS) na
yatafungwa Juni 30.
Serikali
imetenga kiasi cha Sh bilioni 306 kwa
ajili ya mikopo ya wanafunzi 98,000 wa vyuo vya elimu ya juu nchini, ikiwa
wanafunzi wapya na wanaoendelea na masomo.
“Wanafunzi wanaotaka kutuma maombi yao ni
vyema wakatumia muda huu uliobaki, kwani Bodi haitatoa muda wa nyongeza kwa
watakaochelewa kutuma maombi yao,” alisema.
Akizungumzia
hatua ya Bodi kufungua ofisi ya Kanda ya Ziwa, mkoani Mwanza, Mwaisobwa alisema
hii ni katika kutekeleza mikakati ya Bodi katika kusogeza huduma karibu na
wananchi.
“Mpango
mkakati wetu wa miaka mitano kuanzia mwaka 2010, ilikuwa ni kufungua ofisi za
kanda katika kuongeza ufanisi katika kuwahudumia na kusogeza huduma kwa
wananchi, na mpaka sasa tumefungua ofisi za kanda tatu.”
Mbali
na ofisi ya Mwanza itakayohudumia mikoa sita ya Simuyu, Geita, Shinyanga,
Kagera, Mara na Mwanza yenye, pia Bodi ina ofisi katika Kanda ya Kati yenye
ofisi Dodoma na Zanzibar.
Alisema
ofisi ya Mwanza itakuwa inafanya majukumu yote ikiwamo ya utoaji mikopo kwa
wanafunzi wenye sifa waliodahiliwa na urejeshwaji wa mikopo kwa wanufaika wa
mikopo hiyo.
“
Ofisi hii itasaidia sana wananchi ambao walikuwa wakilazimika kutumia siku
nyingi kufika ofisi zetu Dar es Salaam kupata huduma, lakini sasa watahudumiwa
huko huko,” alisema.

No comments:
Post a Comment