Friday, June 20, 2014

SELOUS SASA ENEO LA URITHI WA DUNIA LILILO HATARINI


Pori la Akiba la Selous lenye ukubwa wa kilometa za mraba 50,000 limeingizwa katika  orodha ya maeneo ya Urithi wa Dunia yaliyo hatarini. 
Uamuzi huu umefikiwa katika Mkutano wa 38 wa Kamati ya Urithi wa Dunia unaoendelea jijini Doha, Qatar, ambayo juzi iliyarejeshea hadhi magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara yaliyokuwa hatarini kutoweka kwenye Urithi wa Dunia. 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa vyombo vya habari jana, Uamuzi wa kuingiza Pori la Selous kwenye orodha ya maeneo ya Urithi wa Dunia yaliyo hatarini unalenga kuongeza uelewa wa jamii kitaifa na kimataifa kuhusu matatizo yanayolikabili eneo hilo ili kuwezesha upatikanaji wa misaada ya hali na mali ili kulirejesha katika hadhi yake ya asili. 
Imeeleza kuwa, tangu Pori la Selous lilipowekwa kwenye orodha maeneo ya Urithi wa Dunia, hali yake kwa ujumla iliendelea kuwa nzuri na ya kuridhisha. Hata hivyo, kuanzia mwaka 2010 hali ya pori pamoja na maeneo mengine nchini yamekumbwa na wimbi kubwa la ujangili, hususani wa tembo, hivyo kusababisha kupungua kwa idadi ya tembo katika mfumo ikolojia wa Selous, kutoka tembo 70,000 mwaka 2006 hadi kufikia tembo 13,084 mwaka 2013.
Pori la Akiba la Selous ni mojawapo kati ya maeneo saba yaliyo kwenye orodha ya Urithi wa Dunia nchini. Maeneo mengine ni Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Magofu ya Kilwa Kisiwani na Magofu ya Songo Mnara, Michoro ya Miambani ya Kondoa, na Mji Mkongwe Zanzibar. 
Malengo makuu na faida ya kuweka eneo kwenye orodha ya Urithi wa Dunia ni pamoja na kuwa na nguvu ya pamoja kimataifa ya kusimamia uhifadhi wa eneo; kujulikana kimataifa kama kivutio chenye sifa maalum cha utalii; kutumika kwa tafiti mbalimbali za uhifadhi pamoja; na kuvutia misaada ya kimataifa ya kiuhifadhi.
Kwa uamuzi huo, Kamati ya Urithi wa Dunia imetoa mwaka mmoja kwa Serikali ya Tanzania kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa kukomesha ujangili wa tembo katika Pori la Akiba la Selous na hatimaye kuliondoa kwenye orodha ya maeneo ya urithi wa dunia yaliyo hatarini. 
Tayari Ujerumani imeahidi kutoa Euro milioni moja (Sh bilioni 2.1)  na kuhimiza mataifa mengine yatoe misaada ya kifedha na kiufundi kwa Tanzania ili kukabili haraka tatizo hilo sugu.  Mataifa mengine yakiwemo Ureno, Algeria, Senegal, Lebanon na Colombia yameungana na Ujerumani, kuhamasisha Jumuiya ya Kimataifa kuisaidia Tanzania kutimiza azma yake.

No comments: