Vitambulisho vya kupiga kura nchini, vitatolewa upya kwa
wananchi wote, ikiwa ni sehemu ya mchakato wa kuboresha daftari la kudumu la
wapigakura.
Mchakato huo wa kutoa vitambulisho upya, utakaotekelezwa
Septemba mwaka huu, utagharimu Sh bilioni 293 .
Tofauti na vitambulisho
vya awali vya karatasi vilivyotolewa kwa mara ya kwanza mwaka 2004, vipya
vitakuwa vya plastiki. Vimebadilishwa kutokana na matumizi ya teknolojia mpya
katika uandikishaji.
Teknolojia itakayotumika ni ya Biometric Voter Registration
(BVR), ambayo inachukua au kupima taarifa za mtu za kibaiolojia au tabia ya
mwanadamu na kuzihifadhi katika Kanzidata (database) kwa ajili ya utambuzi.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu
Damian Lubuva, alisema hayo jana wakati akifungua mkutano kati ya tume na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari,
kuhusu uboreshwaji wa daftari la wapiga kura.
Alisema katika
uboreshaji huo, wapigakura wa zamani,
kwa maana waliokuwa kwenye daftari la sasa,
watatakiwa kwenda katika vituo vya kujiandikisha kuchukuliwa taarifa zao hasa alama za vidole,
picha na saini zao katika mfumo mpya wa BVR na hatimaye kupewa vitambulisho
vipya.
Alisema vitambulisho hivyo vipya, vitatolewa papo hapo
uandikishaji ukikamilika na vitakuwa vya plastiki ngumu na namba ya mpigakura
itakayoonekana kwenye kitambulisho hicho, itakuwa ni ya kudumu na pekee kwa
mpiga kura husika.
“Vitambulisho hivi vitatumika kupiga kura katika uchaguzi mkuu
ujao pamoja na kura ya maoni ya Katiba mpya na kuhitimisha matumizi ya
vitambulisho vya wapiga kura vya awali,”
alisema Lubuva.
Akiwasilisha mada katika mkutano huo kuhusu maandalizi hayo
kwa kutumia mfumo wa BVR, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Julius Malaba alisema
wapigakura watakaokuwa na kadi za zamani, watatakiwa kwenda na kadi hizo katika
kituo cha kujiandikisha kurahisisha kuhamisha taarifa zao za awali katika mfumo
mpya.
“Hata hivyo, kupotea ama kuharibika kwa kadi ya awali,
hakumzuii mpiga kura kwenda kituoni kujiandikisha na kupewa kadi mpya,”
alisema.
Alisema kundi lingine litakalohusika katika uboreshwaji huo ni
watu ambao ifikapo siku ya uchaguzi mkuu
mwakani, watakuwa wametimiza umri wa miaka 18. Pia, wale ambao hawakuwahi kujiandikisha katika
madaftari yaliyopita kwa sababu mbalimbali, watahusika katika uboreshaji wa
daftari.
Alisema baada ya kukamilika kwa uboreshwaji huo, daftari la
awali litawekwa wazi katika maeneo husika na tarehe za ukaguzi, zitatangazwa
ili kila aliyejiandikisha kwenda kukagua na kuona kama taarifa zake,
zimeandikwa na kuchukuliwa kwa usahihi.
“Kipindi hicho pia kinatoa nafasi kwa wapigakura
waliojiandikisha katika kata kuweka pingamizi kwa wale watakaoonekana
wameandikishwa katika daftari lakini hawana sifa kama wasiokuwa raia au
wasiotimiza umri unaotakiwa kisheria,” alisema.
Alisema matumizi ya mfumo wa BVR, yataweza kutoa majibu kwenye
changamoto zilizojitokeza katika mifumo mingine iliyotangulia na kuwezesha kuondoa wapigakura,
waliojiandikisha zaidi ya mara moja, kutambua wapigakura siku ya uchaguzi na
kuhamisha wapigakura waliohama.
Hata hivyo, Lubuva alisema
mfumo huo wa BVR utatumika kwa
ajili ya kuandikisha wapigakura pekee na
si kwa ajili ya kupiga kura kielektroniki au vinginevyo.
Alisema matumizi ya mfumo huo, yametokana na changamoto
zilizojitokeza katika matumizi ya Optical
Mark Recognition (OMR) na kufanya daftari la kudumu la wapigakura kuwa na
kasoro na kusababisha wadau wa uchaguzi kuhoji uhalali wake.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari, Lubuva alisema vifaa
kwa ajili ya kazi hiyo vimekwishaagizwa. Tume itavipokea Agosti mwaka huu ili
kuanza uboreshaji huo huku vifaa vichache kwa ajili ya mafunzo kwa watendaji
vitapokewa mwezi Julai na kuanza mfunzo hayo.
Alisema kwa sasa uandikishaji utafanyika katika ngazi ya
vitongoji, vijiji na mitaa, tofauti na awali ambapo vilikuwa katika ngazi ya
mtaa.
Sasa vituo vya kujiandikishia, vimeongezeka kutoka 24,919 hadi 40,015 ili kuwa karibu na
wananchi na kuongeza mwamko wa kujiandikisha na kupiga kura. Mchakato wa
uandikishaji ukianza, huduma zitakuwepo kwa siku 14 kituoni.
Alisema maandalizi ya awali yamekamilika, kinachofuata ni
mafunzo na kuanza uboreshwaji wa daftari utakaogharimu Sh bilioni 293 wanazopata
kutoka serikalini na tayari sehemu ya fedha, wameshapokea na kutumika kukagua
vituo .
Naibu Katibu wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
na Tehama, Dk Sist Cariah,
akizungumzia suala la vitambulisho vya taifa na hivi vya wapigakura,
alisema vitambulisho hivyo ni tofauti kwani wao wanatoa kwa ajili ya kukamilika
kwa muda maalumu lakini vile vya taifa ni endelevu.
Alisema kwa sasa, vitambulisho vya taifa hawajakamilisha kutoa hata Dar es Salaam pekee hivyo ni
vigumu kutumika kwa uchaguzi ujao na kura ya maoni kwa Katiba mpya lakini
wakikamilisha vitambulisho vya taifa , vitatumika katika uchaguzi.
Alisema katika mfumo huo mpya, watawasiliana na Wakala wa
Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) kuweza kuwaondoa wote waliofariki kwa
kutumia takwimu za hospitalini na vyeti vya vifo vitakavyotolewa.

No comments:
Post a Comment