Maeneo mbalimbali visiwani Zanzibar, yamepangwa kuwekwa kamera
za CCTV, kukabili matukio ya uhalifu.
Waziri wa Habari, Utangazaji, Utalii na Michezo, Said Ali
Mbarouk amesema mchakato wa utafiti wa kuweka
kamera hizo, umekamilika na kipaumbele ni eneo la Mji Mkongwe.
Mbarouk alisema hayo wakati akijibu hoja mbalimbali za wajumbe
wa Baraza la Wawakilishi, waliochangia makadirio mapato na matumizi ya bajeti
ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2014/2015 katika Baraza Wawakilishi.
Alisema kampuni mbili, zilipewa kazi hiyo ya kuweka kamera za CCTV katika maeneo
mbalimbali , ambapo kipaumbele ni Mji Mkongwe wa Zanzibar.
“Mheshimiwa Naibu Spika, kampuni hizo tayari zimewasilisha
taarifa yake serikalini kwa ajili ya uchambuzi wa kina na ripoti yake
itatangazwa kwa wananchi,” alisema.
Alisema uwekaji wa kamera za CCTV ni muhimu kwa ajili ya
kukabili matukio ya uhalifu vitendo vya uhalifu ambavyo huathiri maisha ya watu
na maendeleo ya sekta ya utalii.
Mwakilishi wa Mji Mkongwe,
Ismail Jussa Ladhu alitaka kufahamu mikakati ya kuweka kamera za CCTV za
kurekodi matukio mbalimbali , ikiwemo ya uhalifu katika eneo la Mji Mkongwe.
Jussa alisema kama mradi huo wa kuweka kamera ungekamilika na
kufanya kazi, matukio mengi ikiwemo
kumwagiwa tindikali kwa raia wawili wanawake kutoka Uingereza, kungedhibitiwa
na wahusika wangekamatwa.
Awali, Mbarouk alisisitiza suala la kuimarishwa kwa amani na
utulivu nchini na alitaka jamii kuachana na vitendo vya uhalifu ambavyo ni
tishio kwa maisha ya watu.
Alisema matukio mbalimbali ikiwemo ya hivi karibuni la
kulipuliwa bomu eneo la Darajani, kunatishia amani ya nchi pamoja na wageni
kutembelea Zanzibar.
“Sekta ya utalii inategemea sana amani na utulivu na
ikivurugika tu, basi hakuna mgeni atakayezuru Zanzibar katika mazingira ya
vurugu na fujo,” alisema.
Wakati huo huo, Mwakilishi wa Viti
Maalumu, Asha Bakari Makame, alisema kutokana
na kuwepo matukio ya ugaidi, suala la watu kupekuliwa zaidi, hususani wanawake
waliovaa baibui ni jambo la kawaida.
Alisema yapo matukio ya
wanawake, kutumia vibaya mavazi hayo, kutokana na wengine kuficha sura zao kwa
lengo la kufanya uhalifu huo.
“Mimi sipingi matumizi ya kivazi cha baibui...lakini kufuatia
kuibuka kwa matukio ya uhalifu na vitendo vya ugaidi, wanawake waliovaa mabaibui wanalazimika
kupekuliwa,” alisema.
Alisema mbinu za uhalifu zimeongezeka siku hizi hali ambayo
pia wanaume wanaweza kutumia vazi hilo
kwa ajili ya kutekeleza uhalifu.
Vazi hilo ambalo ni maarufu kwa wakazi wa mwambao wa pwani ya Afrika ya Afrika,
hususani Zanzibar, lilizua mjadala jana kwenye Baraza la Wawakilishi baada ya
baadhi ya wajumbe wanawake, kulalamika kwamba wanaofanya kazi kwenye vyombo vya
habari vya Serikali ya Zanzibar, wanalazimishwa kuvua mavazi hayo wanapoingia
kazini.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Habari, Utangazaji, Utalii na
Michezo, Bihindi Khamis Hamadi alisema
uvaaji baibui kwa wanawake, wanapokuwa
kazini ni upendeleo na si
utaratibu wa kazi.
Alisema utaratibu wa kazi na masharti yake, upo wazi kwamba
vazi hilo haliruhusiwi kuvaliwa sehemu ya kazi.
“Mheshimiwa Naibu Spika yapo malalamiko mengi kutoka kwa
wafanyakazi wa Serikali kwamba wanazuiliwa kuvaa mabaibui katika sehemu ya
kazi...ukweli unabakia kuwa, vazi la baibui kazini haliruhusiwi na
kinachofanyika ni mazoea tu kwa wanawake
hao,” alisema.
Alikiri pamoja kwamba ni sehemu ya utamaduni wa wananchi wa
Zanzibar, wanawake wanapoingia kazini na mavazi hayo, hutakiwa kuyavua na kuyahifadhi katika sehemu
maalumu hadi wanapoondoka kazini.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, jana aliliambia Bunge mjini Dodoma
kwamba matukio ya uhalifu yanayotokea Zanzibar, ikiwemo kumwagia viongozi tindikali na utumiaji wa
mabomu ya kurusha kwa mkono, yalipangwa kuwa mengi zaidi, lakini Serikali
imeyadhibiti.
Alisema hayo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti
Maalumu, Betty Machangu (CCM).
Pinda alisema baada
ya matukio hayo Zanzibar, Serikali
ilijipanga vizuri ikiwemo kutumia vyombo vya kimataifa, kujua chanzo cha
matukio hayo na katika harakati hizo, walibaini kulikuwa kutokee matukio mengi
zaidi, Serikali ikayazuia.
Katika swali lake
kwenye kipindi cha Maswali ya Papo kwa Hapo kwa Waziri Mkuu, Machangu alitaka
kauli ya Serikali kuhusu kuibuka kwa vikundi vya kihalifu vya vijana na vingine
vyenye tabia ya kigaidi.
Alitaja baadhi ya
vikundi hivyo ni Panya Road, Kiboko Msheli, Komando Yosso na Toto Tundu, na
vingine vilivyotokea Mtwara ambavyo vilikuwa vikipewa mafunzo vichakani na
kwamba yako madai, baadhi walipelekwa Somalia.
Machangu pia alitaka
kufahamu kauli ya Serikali kuhusu matukio ya Zanzibar kuhusu mauaji ya padre na
kumwagiwa tindikali kwa mashekhe.
Katika ufafanuzi wake,
Pinda alisema Machangu amechanganya mambo mawili katika swali lake, moja la
ugaidi na lingine la uhalifu wa kawaida.
Katika suala la uhalifu
la vikundi hivyo kupora vitu na kukimbia, Polisi imeshafanyia kazi. “Pale Dar
es Salaam hali sasa ni shwari. Naomba vijana wajiepushe na vitu
vitakavyowakutanisha na mkono wa dola,” alisema.
Pinda ametoa kauli hiyo, wakati mwishoni mwa wiki iliyopita
mtu mmoja alifariki dunia na wengine saba kujeruhiwa baada ya kurushiwa bomu na
watu wasiojulikana katika eneo la Darajani, muda mfupi baada ya kuhudhuria
mawaidha yaliyokuwa yakitolewa na Shekhe Kassim Mafuta Kassim (38) mkazi wa
Pongwe mkoani Tanga. Aliyefariki dunia kwa bomu hilo ni Muhammed Khatib Mkombalaguha.
Tukio hilo la mlipuko ni la nne kutokea mwaka
huu. Mengine ni yaliyotokea Kanisa la
Evangelist lililopo maeneo ya Fuoni Machi 2, Kanisa la Anglikana, Mkunazini,
Februari 24 na mlipuko mwingine ulitokea kwenye hoteli ya kitalii ya Mercury
ilioko Forodhani. Vilevile, Zanzibar imeandamwa na matukio ya kumwagiwa watu
tindikali pamoja na kushambuliwa kwa risasi.

No comments:
Post a Comment