Mahakama nchini Marekani imetoa uamuzi kwamba Mtanzania,
Khalfan Khamis Ghailan (40), aliyefungwa kifungo cha maisha kwa mashambulizi dhidi
ya Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam, ana haki ya kuwasiliana na ndugu
zake.
Akisoma uamuzi wa kesi hiyo, Jaji Marcia Krieger alisema
marufuku ya mawasiliano aliyowekewa kijana huyo, haikuwa na mashiko ya kisheria
na yalikosa ushahidi wa kuithibitisha.
Katika hukumu yake ya kurasa 45, Jaji Krieger alisema
hakuridhishwa na ushahidi kutoka Ofisa wa Shirika la Upelelezi la Marekani
(FBI) kwamba Khalfan amekuwa akigoma kula, kutoa kauli mbaya dhidi ya Marekani
na kuwazulia uongo wafanyakazi wa jela.
Jaji huyo aliliamuru Shirika la Upelelezi la FBI na maofisa wa
Jela, kupitia upya orodha ya majina ya watu, ambao wanaweza kuwasiliana naye.
Kaka wa Khalfan, Rubea Khamis aliyeko Zanzibar alikaririwa
akisema: “Hukumu hii ina maana kubwa kwa familia yetu, ataweza kuzungumza na
watoto na jamaa zake ambao wamekuwa wakimjua kupitia hadithi tu."
Ghailan alikuwa
ameishitaki FBI na Idara ya Magereza ya nchi hiyo, kwa kumzuia kuwasiliana na
ndugu na marafiki zake kadhaa, akiwamo mmoja wa kaka zake, akihoji kwamba
marufuku hiyo ni kinyume cha Katiba ya Marekani.
Kijana huyo alitiwa
hatiani kwa kuwa sehemu ya mtandao wa kigaidi wa kundi la al-Qaida na amefungwa
kwenye gereza lililopo jimbo la
Colorado, linalotajwa kutumika kufunga
watu wanaominika kuwa hatari.

No comments:
Post a Comment