Katika
jitihada za kufufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), upo mpango wa kununua
ndege sita, hatimaye liwe na ndege nane zitakazokuwa zikitoa huduma ya
usafiri nchini.
Naibu
Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba, alisema hayo jana bungeni alipokuwa
akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Lucy Owenya (Chadema).
Katika
swali lake, Owenya, alitaka kufahamu ATCL inamiliki ndege ngapi na kati ya
hizo, ni ngapi zimekodishwa na zinafanya safari kwenda wapi.
Baada
ya kujibiwa kwamba ndege inayomilikiwa na ATCL ni moja, Owenya alisema ni aibu
kwa shirika kuwa na ndege moja wakati liliwahi kumiliki ndege saba.
Ili
kuondoa aibu hiyo, Mbunge huyo alipendekeza mali za shirika hilo, zikiwemo
nyumba zake katika nchi mbalimbali, ikiwemo ya London, Uingereza, ziwekwe
rehani ili kupata mkopo wa kununua ndege hizo.
Pia
alipendekeza njia za ATCL kwenda katika nchi mbalimbali, hususani ya Dubai, katika nchi za Falme za
Kiarabu, Uingereza na Marekani, zikodishwe
kuongezea shirika hilo fedha za kujiendesha kwa kuwa kwa sasa halina
uwezo wa kutumia njia hizo.
Akifafanua
mipango ya Serikali ya kufufua shirika hilo, Dk Tizeba alisema mbali na
kumiliki ndege hiyo moja aina ya Dash 8 Q 300 yenye uwezo wa kubeba abiria 50,
ATCL pia imekodi ndege moja aina ya CRJ 200, yenye uwezo wa kubeba watu 50
kutoka Kampuni ya AXMAX ya Kenya.
Kwa
mujibu wa Dk Tizeba, ndege inayomilikiwa na ATCL, inatoa huduma zake katika
njia za Dar es Salaam, Kigoma, Mtwara na Bujumbura, nchini Burundi.
Aidha ndege iliyokodishwa, inatoa huduma zake
katika njia za Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Mtwara na Hahaya nchini Comoro.
Hali ya sasa ya ATCL, ni tofauti na ilivyokuwa
miaka michache iliyopita ambapo haikuwa na ndege hata moja iliyokuwa ikitoa
huduma.
Mwaka 2011, aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi,
Omari Nundu, akijibu swali la Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR
Mageuzi) bungeni, alisema ATCL ilianzishwa kwa kupewa ndege 11 mwaka 1973,
lakini mpaka mwaka huo 2011, hakukuwa na ndege hata moja iliyokuwa ikifanya
kazi.
Akifafanua mipango ya Serikali ya hivi
karibuni, Dk Tizeba alisema ATCL ina mpango wa kununua ndege mbili, kwa mfumo
wa kibiashara wa kukodi huku malipo ya ununuzi yakifanyika taratibu.
Ndege
hizo aina ya D8 Q 400, zenye uwezo wa kubeba abiria 78 kila moja baada ya
kununuliwa, zitaongeza wigo wa huduma za ATCL katika njia za Nairobi nchini
Kenya, Kigali nchini Rwanda na nchini Uganda.
Kwa
mujibu wa Dk Tizeba, ununuzi wa ndege
hizo utafanyika baada ya kukamilika kwa taratibu za kisheria na kibiashara
ambazo zinafuatwa hivi sasa, ili ndege hizo zianze kufanya kazi mwishoni mwa
mwaka huu.
Baada
ya kukamilika kwa utekelezaji wa mpango huo, ambao utafanya ATCL kurusha ndege
nne na kutoa huduma za ndani na katika nchi za Afrika Mashariki, Dk Tizeba
alisema utafuata utekelezaji wa ununuzi wa ndege nyingine mbili.
“Kuna
mpango wa kununua ndege mbili ndogo aina ya Y12E, kwa mkopo nafuu wa Exim Bank kutoka China
kwa Serikali ya Tanzania, kila moja ina uwezo wa kubeba abiria 20”, alisema.
Mbali
na ndege hizo, pia Serikali kwa mujibu wa Dk Tizeba itanunua ndege mbili aina
ya ERJ 170 na ERJ 190, zenye uwezo wa kubeba abiria 80 mpaka 100 kutoka nchini
Brazil.
“Ndege
hizi zitanunuliwa kwa utaratibu wa mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Brazil,”
alisema Dk Tizeba na kusisitiza kuwa baada ya kupatikana kwa ndege hizo, ATCL
itaanza kutumia njia zake za kimataifa kwa kuwa bado zipo.

No comments:
Post a Comment