Friday, June 20, 2014

TRENI YA BARA KUANZA TENA SAFARI ZAKE


Treni ya abiria ya bara inatarajiwa kuanza tena huduma zake wiki ijayo baada ya kukamilika ukarabati wa daraja eneo la Bonde la Mto Ruvu, mkoani Pwani.
Taarifa iliyotolewa na uongozi wa  Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) jana, imesema safari zitaanza Jumanne, ijayo saa 11 jioni kutoka Stesheni ya Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Ofisi ya Uhusiano ya TRL kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji ,  Elias Mshana, muda wa kuondoka treni kwa siku za Jumanne na Ijumaa kutoka Stesheni ya Dar kwenda Kigoma na Mwanza utakuwa saa 11 jioni.
Aidha muda wa treni ya kutoka Kigoma na Mwanza kwenda Dar es Salaam katika siku za Alhamisi na Jumapili ni saa 11 jioni  kutoka Kigoma na saa 12 jioni  kutoka Mwanza.
Uongozi huo umeshukuru wateja wake kwa ushirikiano na uvumilivu waliouonesha wakati wakisubiri kukamilika kwa kazi ukarabati wa njia ya reli baada ya safari kutangazwa kusitishwa hivi karibuni.
Katika hatua nyingine, huduma za usafiri wa treni ya abiria jijini Dar es Salaam zimesitishwa kwa muda tangu jana  kwa sababu zilizotajwa kwamba ni za kiufundi.
“Uongozi wa TRL unasikitika  kuwataarifu wananchi na wateja wake  wa  huduma ya treni ya Jiji kuwa hiyo  imesitishwa kwa muda wa siku tatu kuanzia kesho (jana)  hadi  Jumammosi (kesho). Aidha huduma hiyo itaanza tena hapo Jumatatu kwa kufuata ratiba yake ya kawaida,” ilisema taarifa ya uongozi.
Uamuzi huo unatokana na sababu za kiufundi ikiwemo kufanyiwa matengenezo vichwa vyote viwili ambavyo vimekuwa vikihudumia treni hiyo ya Jiji.
Taarifa hiyo ya ofisi ya Uhusiano ya TRL, ilisema vichwa hivyo vinapaswa kufanyiwa ukarabati katika Karakana Kuu ya TRL Morogoro na kwamba vitarejeshwa jijini keshokutwa.

No comments: