Kampuni ya ujenzi ya Strabag International GmbH inayojenga
barabara ya Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (Dart) imetangaza kufungwa kwa
baadhi ya njia katika eneo la taa za Ubungo, Dar es Salaam kuanzia leo usiku hadi keshokutwa kwa ajili ya kuruhusu
ujenzi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam,
Ofisa Uhusiano wa Dart, Yahya Mkumba,
alisema kazi hiyo itahusu ujenzi katika
makutano ya barabara za Morogoro, Sam Nujoma na Nelson Mandela katika eneo
hilo.
Kutakuwa na awamu mbili za ufungaji wa njia kuanzia leo saa 4
usiku hadi keshokutwa saa 12 asubuhi;
kwa ajili ya kutoa nafasi kwa ujenzi unaoendelea.
Akielezea zaidi,
alisema katika awamu ya kwanza, ujenzi huo utahusisha eneo la upande wa
kulia la makutano ya barabara ya Sam Nujoma na Morogoro ambalo litafungwa.
“Hali hii itasababisha magari yanayotoka maeneo ya Buguruni na
Tabata kuelekea maeneo ya Mwenge kutoweza kutumia njia ya Sam Nujoma
watakapofika taa za Ubungo,” alisema.
Alifafanua kuwa magari hayo yatalazimika kufuata alama
zitakazowaelekeza kupita katika barabara za mradi zinazojengwa hadi barabara ya
Shekilango ambapo wataweza kukutana tena na Sam Nujoma kwa kutumia barabara ya
Igesa.
Pia magari yatakayokuwa yanatoka Sinza kupitia barabara ya
Igesa hayataweza kwenda eneo la Ubungo
yatakapofika katika makutano ya barabara za Igesa na Sam Nujoma.
Alifafanua kuwa magari yanayotumia Barabara ya Morogoro kutoka
maeneo ya Mbezi na Kimara, yatalazimika
kuchepuka kulia na kutumia barabara za mabasi ya mwendo wa haraka yatakapofika
eneo la Kibo ambapo patakuwa na kizuizi.
Mkumba alisema katika awamu ya pili ya ujenzi huo, eneo la
upande wa kushoto la makutano ya barabara za Morogoro na Nelson Mandela
litafungwa kesho kuanzia saa nne usiku hadi keshokutwa saa 12 asubuhi.
Katika awamu hii, alisema, watumiaji wa magari yatakayokuwa
yanatokea eneo la Mwenge kutumia barabara ya Sam Nujoma yatalazimika kuchepuka
kushoto kukamata barabara ya Igesa kisha Shekilango.
Pia magari yatakayokuwa yanatoka Barabara ya Mandela na kutaka
kwenda mjini kwa kutumia njia ya Morogoro yatalazimika kuchepuka kushoto na
kwenda kugeukia eneo la Kibo ili kukamata barabara ya Morogoro.
“Tunaomba radhi kwa usumbufu wowote utakaotokea,” alisema Mkumba na kuongeza kwamba anaamini kutakuwa
na usumbufu ambao hata hivyo utakuwa ni wa muda.
Mradi
wa Mabasi yaendayo Haraka unaoendelea, unatarajiwa baada ya kukamilika
utaondoa adha ya foleni katika Jiji la
Dar es Salaam na kuleta ufanisi wa usafiri.

No comments:
Post a Comment