Friday, June 20, 2014

KAMPUNI ZA GESI ZAITWA KUTOA HUDUMA VIJIJINI

Kampuni mbalimbali zinazojishughulisha na uuzaji wa mitungi ya gesi za kupikia zimetakiwa kupeleka huduma zao vijijiji.
Mwito huo ulitolewa juzi na Naibu Kamishna kutoka Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia gesi asilia, Robert Kahiza wakati akizindua mitungi mipya ya gesi ya kupikia iliyobuniwa na Kampuni ya Lake Gas. 
Kahoza alisema kuwa kwa sasa wananchi wa vijiji mbalimbali wanatumia kuni na wanashiriki kwa kiasi kikubwa kwenye uharibifu wa mazingira. 
Alisema kuwa uharibifu huo ni mkubwa na unachangia kwa kiasi kikubwa suala zima la mabadiliko ya tabia nchi na kuleta athari nyingine nyingi. 
Alisema kuwa iwapo kampuni nyingi zaidi zitajitokeza na kupeleka gesi mikoani na hasa vijijini zitawawezesha wananchi kuepuka matumizi ya kuni. 
"Najua tatizo kubwa hapa si wananchi kushindwa kutumia gesi kupikia ila kilichopo ni upatikanaji wa gesi katika maeneo ya vijijini, iwapo wakipelekewa gesi na kuwezeshwa kuitumia ni dhahiri kuwa hawatakata kuni kwa matumizi ya umeme,"alisema Kahiza. 
Kwa upande wake ‎Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Lake Oil inayomiliki na kusambaza gesi ya Lake Gas, Ally Edha Awadh alisema kuwa kampuni yake imejipanga kuifanyia kazi changamoto hiyo kwa kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya gesi ya kupikia inafika vijijini.
Alisema kuwa mitungi hiyo mipya iliyozinduliwa juzi ni ya kisasa na inasaidia kwa kiasi kikubwa urahisi katika kutumia.

No comments: