Serikali kupitia Bodi ya Pamba imetangaza bei elekezi ya
ununuzi wa pamba ambayo ni Sh 750 kwa
kilo katika msimu wa mwaka 2014/15.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo, George Wasira alisema msimu uliopita bei elekezi
ilikuwa Sh 700 kwa kilo na kwamba ongezeko hilo la Sh 50 limefikiwa na wadau wa
zao la pamba nchini kutokana na kuporomoka kwa bei ya zao hilo katika Soko la
Dunia.
Bei hiyo ilitangazwa juzi wakati wa uzinduzi wa msimu mpya wa
ununuzi wa pamba uliofanyika kitaifa katika kijiji cha Isole wilayani Sengerema mkoani Mwanza.
“Baada ya tathmini ya
kina kufanyika iliyolenga kulinda maslahi ya wadau wote yaani wakulima na
wanunuzi, bei elekezi itakuwa Sh 750,” alisema Wasira
Hata hivyo bei hiyo elekezi haikupokewa kwa furaha na wakulima
wa zao hilo wilayani Sengerema kwa madai kuwa wamekuwa wakitumia gharama kubwa
katika uzalishaji halafu wanauza kwa bei ndogo.
Miongoni mwa waliozungumza kwenye uzinduzi huo, walisema
wamekuwa wakitumia gharama kubwa kwenye
uzalishaji kuanzia kulima, dawa za kunyunyuzia pamoja na palizi hivyo bei hiyo
elekezi inawanyonya.
Akizindua msimu wa
ununuzi wa pamba 2014/2015, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Baraka Konisaga alionya wanunuzi wa pamba wanaowaibia
wakulima kwa kutumia mizani.
Aidha taarifa zinaonesha uzalishaji wa zao hilo nchini unatarajiwa kuongezeka msimu huu kutoka kilo
milioni 245 mwaka 2013/2014 hadi kufikia
kilo milioni 250.
No comments:
Post a Comment