Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni Amiri Jeshi
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama nchini, amesema anatarajia kurejea
darasani kushika tena chaki, kwa kuwa Mhadhiri kwenye Chuo cha Taifa cha Ulinzi
(NDC) jijini Dar es Salaam.
Rais Kikwete alisema hayo jana mchana
wakati alipotoa Mhadhara kuhusu Usalama
wa Taifa, mbele ya wanafunzi wa Chuo hicho kilichoko Kunduchi.
Aliwaambia wanafunzi wa kozi ya pili ya
chuo hicho kutoka nchini na nchi za jirani za Uganda, Kenya na Rwanda;
“Najisikia mwenye raha sana kuweza kurudi darasani kutoa mhadhara huu. Tukio
hili linanikumbusha enzi zangu katika Chuo cha Kijeshi cha Monduli (TMA). Ni
matarajio yangu pia kuwa nitaweza kurudi kuwa mhadhiri katika chuo hiki baada
ya kukamilisha kazi yangu ya sasa.”
Rais Kikwete ambaye alizungumza kwa kiasi
cha saa mbili, alianza mhadhara wake baada ya kupata maelezo kuhusu maendeleo
ya chuo hicho na baadaye akajibu maswali ya wanafunzi, ambao walimuuliza kuhusu
mambo mbalimbali yanayohusiana na usalama wa nchi.
NDC ilianzishwa rasmi Septemba 2, mwaka
2012 na chuo hicho kilizinduliwa na Rais Kikwete Septemba 10, mwaka huo huo,
2012 wakati alipotembelea chuo hicho kwa mara ya kwanza, kufuatia juhudi kubwa
za uongozi wake kuhakikisha kuwa chuo cha namna hiyo na cha aina yake
kinaanzishwa nchini. Rais pia alifungua kozi ya kwanza ya chuo hicho.
Kundi la wanafunzi wa kwanza kwenye chuo
hicho, lilimaliza mafunzo yake Julai 23, mwaka 2013 na sasa chuo hicho
kinaendesha kozi ya pili yenye wanafunzi 30.
Chuo hicho tayari kimepata usajili kamili
wa NECTA, ambako kina uwezo wa kutoa shahada ya uzamili katika masomo ya
Strategic Studies (Taaluma za Mikakati).

No comments:
Post a Comment