Mkazi wa mmoja wa Kijiji cha Igurubi Tarafa ya
Igurubi Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa
tuhuma za kuwaingilia kimwili watoto wenye umri wa chini ya miaka kumi, baada
ya kuwarubuni kwa kuwapa ubuyu na Sh 500 taslimu.
Hayo yamethibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Suzana Kaganda
aliyesema tukio hilo ni la juzi katika Mtaa wa Muhaya Kijiji cha Igurubi.
Alimtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Sudi Seif
(47). Alisema mtuhumiwa huyo anadaiwa kuwatendea unyama watoto hao, kwa
kuwalaghai kuwapa ubuyu na pesa, endapo wangemkubalia kufanya tendo la mapenzi.
Alisema kwa kuwa watoto hao walikuwa
wadogo, alifanikiwa kuwashawishi, na alianza kwa kumchukua mtoto wa kwanza
mwenye umri wa miaka 5 na miezi 4, anayesoma chekechea Shule ya Msingi Igurubi.
Kamanda huyo aliongeza kuwa, akiwa
chumbani na mtoto huyo alimwingilia kimwili katika sehemu zote za siri na
kumsababishia maumivu makali hadi wazazi wake walipomgundua wakati aliporudi
nyumbani muda wa jioni.
Alidai kuwa baada ya tukio hilo kwa mtoto
wa kwanza, alimchukua mtoto mwingine mwenye umri wa miaka 9 anayesoma darasa la
pili Shule ya Msingi Ikonda Kata ya Igurubi, aliyemfanyia kama mtoto wa kwanza.
Kaganda alisema baada ya matukio hayo,
mtuhumiwa aliendelea kujipumzisha nyumbani kwake, lakini ghafla alivamiwa na
kundi la wanakijiji waliopanga kumdhuru.
Hata hivyo, mtu huyo aliokolewa na askari
wa Kituo kidogo cha Polisi Igurubi, waliomchukua na kumpeleka Kituo kikuu cha
Polisi mjini Igunga.
Kutokana na tuhuma hizo, Kamanda alisema
wanasubiri uchunguzi kutoka kwa daktari ili waweze kumfikisha mahakamani
mtuhumiwa huyo.
Aliwaonya wananchi kuachana na tabia za
aina hiyo, zenye kuondoa utu na haki za watoto wasiokuwa na hatia.
Kaimu Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Wilaya
ya Igunga, Mashaka Hilaly alithibitisha kuingiliwa kimwili kwa watoto hao na
kusema wameharibiwa vibaya katika sehemu zote za siri, hali iliyolazimu
kuwalaza hospitalini.

No comments:
Post a Comment