Mtu
mmoja amekufa na
wengine sita wamejeruhiwa baada ya gari walilokuwa wamepanda kutumbukia kwenye
Daraja la Kinyerezi jijini Dar es
Salaam.
Tukio hilo lilitokea Juni 19 ambapo gari
lenye namba za usajili T142 BJM Scania, likiwa na tela namba T111 ALD,
likiendeshwa na dereva ambaye hajafahamika, lililokuwa likitokea Pugu
Kinyamwezi kuelekea Kinyerezi na mzigo wa tofali ukiwa ndani ya Kontena.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo,
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi alisema gari hilo
lilitumbukia katika daraja hilo baada ya daraja kuvunjika kutokana na gari hiyo kupita kwa nguvu.
Alisema
gari hilo, lilitumbukia kutokana
na dereva kukaidi amri ya walinzi wa daraja, ikiwa ni pamoja na alama za magari
yanayoruhusiwa kupita.
Gari hilo lilikuwa na zaidi ya tani 30.
Katika tukio hilo mbeba mizigo anayekadiriwa kuwa na miaka kati ya 20 na 25,
alikufa papo hapo na wengine sita, watano kati yao ni wabeba mizigo na mmoja ni
fundi walijeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili.
Majeruhi hao ni Simon Kamai (22), Raphael
George (20), Lameck Maliki(22), Chande Mohamed (23), Said Makame (25) na Simon
Ennel (24) ambaye ni fundi ujenzi. Majeruhi walitibiwa katika Hospitali ya
Taifa Muhimbili na waliruhusiwa. Maiti amehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili.
Hali ya usalama imeimarishwa kwa
kushirikiana na Kampuni inayojenga daraja hilo, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu
kwa watumiaji wa barabara, viashiria kwa daraja kama halitumiki kwa sababu ya
kushindwa kulitoa gari hilo jitihada za kumtafuta dereva aliyekimbia baada ya
tukio zinaendelea.

No comments:
Post a Comment