Saturday, June 21, 2014

KESI YA GHOROFA LILILOPOROMOKA KUUNGURUMA JUNI 27


Uamuzi wa ombi la marejeo lililowasilishwa na washitakiwa tisa wa kesi ya mauaji ya watu 27, yaliyotokana na kuporomoka kwa jengo la ghorofa 16, utatolewa Juni 27 mwaka huu katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Washitakiwa hao wanaiomba Mahakama  Kuu ipitie  uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwanyima dhamana bila kupewa haki ya kusikilizwa ili kujiridhisha na usahihi na uhalali. Pia ipitie uamuzi wa kubadilishwa kwa mashitaka kutoka kuua bila kukusudia na kuwa ya kuua kwa kukusudia.
Shauri hilo lilitajwa jana mbele ya Jaji Salvatory Bongole ambaye alisema atatoa uamuzi wa ombi hilo pamoja na pingamizi la awali lililowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) baada ya kupitia hoja za maandishi zilizowasilishwa na pande zote mbili.
Katika ombi lao washitakiwa wanadai upande wa Jamhuri ulibadili mashitaka bila kuijulisha Mahakama mazingira yaliyosababisha wabadilishe, hivyo wanaiomba Mahakama itupilie mbali hati ya mashitaka mapya ya kuua kwa makusudi badala ya kuua bila kukusudia na iamuru wapewe dhamana.
Hata hivyo DPP amewasilisha pingamizi akidai ombi hilo halipo sahihi kisheria,  Mahakama Kuu haina mamlaka ya kusikiliza ombi ambalo kesi yake ya msingi ipo katika hatua ya awali pia ombi hilo linaungwa mkono na hati ya kiapo ambayo ina mapungufu ya kisheria.
Washitakiwa waliowasilisha ombi hilo ni Raza Ladha, Godluck Mbaga, Wilbroad Mugabisyo, Ibrahim Kisoki, Charles Ogare, Zonazea Oushoudada, Michael Hemed, Albert Mnuo na Joseph Ringo. Awali walikuwa wanakabiliwa na mashitaka ya kuua bila kukusudia, wakabadilishiwa mashitaka na kuwa kuua kwa kukusudia.
Inadaiwa kuwa Machi 27 mwaka jana katika mtaa wa Indira Gandhi, washitakiwa waliwaua watu 27 kwa kukusudia kutokana na kuporomoka kwa ghorofa 16. Mshitakiwa mwingine ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala Gabriel Fuime ambaye hajawasilisha ombi hilo.

No comments: