Saturday, June 21, 2014

NHIF KUANZISHA VITAMBULISHO VYA KIELEKTRONIKI


Mfuko wa Taifa  wa Bima  ya Afya (NHIF)  unaandaa  vitambulisho  vipya   vya wanachama  wake vya kielektroniki.
Lengo la hatua hiyo ni kukabiliana na  matumizi  mabaya  ya  vitambulisho  vya sasa,  ambavyo   wanachama  wasio  waaminifu  wanavikodisha  kwa  watu wengine kwa gharama  kubwa  kinyume  cha  utaratibu.
Kaimu Mkurugenzi  Mkuu  wa NHIF, Hamis Mdee  alibainisha hayo  hivi karibuni katika  ufunguzi  wa   mkutano  wa wadau wa NHIF,  uliofanyika  mjini Sumbawanga.
Alisema  baadhi  ya  wanachama wa mfuko  huo  wasio  waaminifu,  wamekuwa  ama  wakiuza  vitambulisho  hivyo au  kuvikodisha,  hususan  kwa watu  wanaosumbuliwa na  magonjwa makubwa, yakiwemo nyonga, figo  na wale  wanaohitaji huduma  ya usafishaji  wa damu.
Kwa mujibu  wa Mdee,  gharama  za  matibabu  ya  baadhi ya magonjwa hayo  makubwa, hufikia zaidi ya Sh  milioni 3.6  kwa mwaka.
Alisema  baadhi  ya  wanachama wa mfuko  huo wasio waaminifu,  huthubutu  kukodisha  vitambulisho  vyao  kwa zaidi  ya Sh  milioni  moja .
Alizitaka  halmashauri  za wilaya na manispaa,  kutengeneza  sheria  ndogo  ili  kujiunga  katika Mfuko  wa Afya ya Jamii (CHF)  iwe ni lazima  badala  ya  hiari. Alisema hatua hiyo itaboresha  uhamasishaji  kwa  wananchi.
Sambamba na   mkutano huo  wa wadau,  pia NHIF  ilitoa  msaada  wa mashuka  180,  ambapo  mashuka  80  yalitolewa kwa Hospitali  Teule ya Manispaa ya Dk Atman  na  100 kwa  Hospitali  ya Mkoa  mjini Sumbawanga.
Kwa upande  wake, Mkuu  wa Wilaya  ya Sumbawanga, Mathew Sedoyeka aliyemwakilisha  Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya  alibainisha kuwa  takwimu  zinaonesha kuwa  hamasa  ya  wananchi kujiunga na CHF, siyo  ya kuridhisha mkoani humo.
“Lakini kwa upande  wa pili,  inawezekana pia  watoa  huduma  mmekuwa ni chanzo  cha  kuwakatisha tamaa  wananchi  wanaojiunga na CHF,  hivyo kusababisha wengine  wasite kujiunga  kutokana na huduma  zisizoridhisha," alibainisha  Sedeyeka.
Akifafanua,  aliongeza kuwa  ni kaya 20,157  kati ya 173,972 , sawa na  asilimia 11.6  zimejiunga  na CHF  mkoani humo  hadi  kufikia Machi 30, mwaka  huu.

No comments: