Serikali
inatarajia kuzalisha ajira 700,000 katika mwaka wa fedha ujao wa 2014/2015,
ikiwa ni sehemu ya kukabiliana na tatizo la ajira.
Waziri
wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka alisema hayo jana wakati akiwasilisha
bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2014/2015
ya Sh bilioni 23.
Alisema
ajira hizo zitapatikana kutokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo,
itakayotekelezwa na taasisi za Umma, Programu ya kukuza ajira kwa vijana pamoja
na hatua za uwekezaji kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC, Mamlaka ya Maeneo Huru
ya Biashara (EPZA) na sekta binafsi.
Kabaka
alisema ili kukuza ajira kwa mwaka huu, wizara imepanga kutekeleza shughuli
mbalimbali ikiwa ni pamoja na kusimamia utekelezaji wa programu ya kukuza ajira
kwa vijana, ambayo imelenga kuwajengea vijana uweo na stadi mbalimbali za kazi
na ujasiriamali.
Alisema
awamu ya kwanza ya miaka mitatu ya utekelezaji wa programu hiyo, itaanza mwaka
huu ambapo Sh bilioni tatu zimetengwa kwa ajili hiyo.
Kabaka
alisema kwa mwaka wa fedha uliopita hadi kufikia Aprili mwaka huu, ajira
630,616 zilizalishwa katika sekta za kilimo ajira 130,974, Elimu 36,073, Ujenzi
na Miundombinu 32,132, Nishati na Madini 453 na
Afya 11,221.
Alisema
TASAF 8686,sekta nyingine za Serikali 2,321 ,sekta binafsi 211,970,viwanda
vidogo na vya kati 7,192,miradi ya uwekezaji kupitia maeneo huru ya uwekezaji
(EPZ) 26,381 mawasiliano 13,619 na kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC) 149,594.
Kabaka
alisema mwaka huu Wizara itaanza utekelezaji wa mfuko wa fidia kwa wafanyakazi,
baada ya kukamilisha kanuni za tozo kwa waajiri wote wa sekta ya umma na
binafsi watachangia katika kuendesha mfuko wa fidia kwa wafanyakazi .
Waziri
Kabaka alisema katika kusimamia ajira kwa wageni na kulinda ajira kwa
Watanzania kwa mwaka wa fedha uliopita ilipokea maombi 7,432 ya vibali vya
ajira za wageni vya daraja B na kati ya maombi hayo 6,237 sawa na asilimia 83.9
yalipewa kibali,1175 yalikataliwa na maombi 20 yalisitishwa kwa uchunguzi.
Akiwasilisha
maoni ya Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya
Jamii, Mwenyekiti wake, Said Mtanda alitaka Serikali kukamilisha mchakato wa
uanzishwaji wa mfuko wa pensheni ya wazee ili wazee nao waboreshewe hali zao za maisha.
Pia,
Kamati ilishauri Serikali kuangalia mfumo wa elimu kwa kufanya utafiti wa kina
wa mitaala iliyopo ili kuona mitaala gani itakayowezesha vijana kujiajiri
wenyewe kwani takwimu zinaonesha vijana
wanaomaliza vyuo vikuu nchini kila mwaka ni 400,000 mpaka milioni moja.
Alisema
lakini wanaopata ajira ni wastani kati ya 80,000 hadi 100,000 katika sekta za
umma na binafsi, suala linaloonekana ajira kwa vijana bado ni tatizo kubwa.
Mtanda
alisema kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia, inakadiriwa vijana 850,000
huingia kwenye soko la ajira kila mwaka nchini huku asilimia 40 ni waliofeli
kidato cha nne.
Alisema
benki hiyo inakadiria kuwa ifikapo mwakani, kutakuwa na ongezeko la vijana
milioni 1.3 katika soko la ajira.
No comments:
Post a Comment