Ikiwa ni takribani mwaka mmoja sasa
tangu Serikali ilipoamua kuanza kutekeleza Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa
(BRN), hatimaye mawaziri wanaotekeleza Mpango huo watawekwa `kikaangoni’ Julai
mwaka huu.
Hayo yalisemwa jijini Dar es
Salaam mwishoni mwa wiki na Mtendaji
Mkuu wa Kitengo cha Rais Kinachosimamia Utekelezaji wa Mpango huo (PDB), Omari Issa alipokutana na watendaji wakuu
kutoka taasisi za umma na binafsi.
PDB iliundwa rasmi Julai mosi mwaka
jana kwa lengo la kusimamia utekelezaji wa miradi mikubwa sita ya kipaumbele
katika sekta za elimu, kilimo, usafirishaji, nishati, maji na ukusanyaji wa
mapato.
“Kazi hii tumeshaitekeleza kwa
takribani miezo 10, tunajiandaa kufanya tathmini ya kina ya utekelezaji ambapo
Julai mwaka huu, mawaziri wote waliosaini mikataba mbele ya Rais Jakaya Kikwete
watahojiwa, watapimwa na matokeo kuwekwa hadharani,” alisema Issa.
Alisema, BRN ni utamaduni unaojaribu
kujenga uwajibikaji, uwekaji wa vipaumbele na kisha kutekeleza mipango husika
kwa wakati bila urasimu uliozoeleka katika sekta nyingi.
Akizungumzia mchakato huo wa kuwapima
mawaziri hao utakavyokuwa, alisema, shughuli hiyo itaanza kwa mawaziri hao
mmoja mmoja kukutanishwa na Rais ambapo atawahoji kwa kina kuhusu kazi
walizopewa na watajieleza.
Mchakato huo utafuatiwa na timu huru ya
tathmini itakayohusisha wataalamu mbalimbali kutoka nje ya nchi ambao nao
wataangalia na kuhakiki utendaji wa mawaziri husika kwa mujibu wa mikakati
waliyopewa kuitekeleza chini ya BRN.
“Zoezi hili litakuwa la wazi kwa kadiri
itakavyowezekana, wananchi wataambiwa nini BRN imeweza kutekeleza na kipi
hakikutekelezwa na sababu zake, ” alisema Issa.
Hata hivyo , alisema mara baada ya
kuhojiwa kwa mawaziri hao mbele ya Rais, (Rais) ndiye mwenye mamlaka ya
kuwachukulia hatua ikiwa ataona kuna haja ya kufanya hivyo kwa kuwa ndiye
aliyewateua.
Akizungumzia mafanikio ya BRN mpaka
sasa, Issa alitaja kuanza kujengeka kwa utamaduni wa watu kuwajibika, kuweka
mipango na kuitekeleza kwa wakati hata
kama miradi hiyo haipo moja kwa moja chini ya BRN.
Alitaja mfano wa sekta ya usambazaji wa
maji kuwa ndani ya miezi 10, tu ya kuanza kwa BRN, zaidi ya Watanzania milioni
2.5 wamefikishiwa huduma hiyo hadi vijijini, wakati kabla ya BRN, kati ya watu
laki tatu hadi tano ndio waliokuwa wakifikishiwa huduma hiyo muhimu.
Watendaji wakuu wengi wa taasisi na
mashirika waliohudhuria walieleza kuridhishwa na BRN na kuahidi kushirikiana nayo katika
kuleta maendeleo ya Taifa.
Tanzania imeanza kutekeleza mfumo wa
BRN Julai mwaka 2013, wenye lengo la kuleta maendeleo na kuifanya nchi kuwa
yenye uchumi wa kati kutoka wa chini na kuwa mfumo huu, uliochukuliwa nchini
Malaysia.
Malaysia wao mfumo huo umeonesha
mafanikio makubwa na sasa ni moja ya nchi iliyoendelea kiviwanda na iko kwenye
rekodi nzuri za nchi zenye uchumi wa juu barani Asia, na inategemewa ifikapo
mwaka 2020 itakuwa ni moja ya nchi zilizoendelea.
Malaysia wakati ikipata uhuru wake,
ilikuwa na uchumi sawa na wa Tanzania, lakini sasa kupitia BRN, mapinduzi ya
maendeleo yameonekana na uchumi wao unaendelea kukua kwa kasi.
Mfumo huo kuanza kutekelezwa hapa
nchini, unaweza kufanikiwa kwa kuwa nchi
ya Malaysia nayo ilikuwa na rasilimali
zinazofanana na za Tanzania kama vile sekta ya
madini na kilimo, ambazo ndizo gurudumu la maendeleo. Nchi nyingine za
Afrika zilizofuata mfumo huo ni Rwanda na Nigeria.
No comments:
Post a Comment