Friday, April 11, 2014

MACHINGA 550 KUPEWA MAFUNZO KANDA YA ZIWA

Wafanyabiashara ndogo 550 wa mikoa mitano ya Kanda ya Ziwa, watanufaika na mafunzo ya biashara na teknolojia ya nishati endelevu, yanayotolewa na shirika lisilo la kiserikali la GVEP.

 Hayo yalielezwa juzi na Meneja wa GVEP, Adam Mbuziba.
Alisema  mafunzo hayo, yanalenga kuzalisha ajira 1200, kusaidia kusimamia biashara 1400, ikiwemo hiyo ya nishati endelevu.
 Alisema tayari wajasiriamali 20 wamewezeshwa
kupata mkopo wa Sh milioni 21  kutoka katika Benki ya Posta, ambapo fedha hizo zitawasaidia kununua vifaa vya kuzalisha umeme wa jua.
“Baada ya kuwapatia mafunzo ya biashara ambayo yatawasaidia kutunza taarifa za fedha tunahakikisha kuwa wanapata mikopo nafuu katika taasisi za fedha kwa kuwawekea dhamana,” alisema.
Alisema tofauti na mafunzo hayo, pia wanapatiwa mafunzo ya jinsi ya kupata masoko, mpango wa biashara na upangaji wa bei, ambayo inaendana na jinsi ya kukokotoa  gharama.
Alisema tangu mradi huu wa kuwasaidia wafanyabiashara wadogo ulipoanza, tayari kuna watu walishaanza kupata mafanikio, kutokana na fursa ya kuwa na nishati hizo, kwa kufanya biashara za
kuchajisha simu vijijini na kuwa na saluni za kunyolea.
Meneja wa Benki ya Posta, Shaban Telatela alisema tangu mradi huo ulipoanza, wameshatoa Sh milioni 45 na hiyo inaonesha jinsi ambavyo wanashirikiana na taasisi ambazo zinawasaidia wajasiriamali wadogo nchini.
Alisema kwa jana, wajasiriamali waliopata mikopo walitoka Wilaya ya Bariadi, Bunda, Sengerema na Mkoa wa Shinyanga.

No comments: