Friday, April 11, 2014

BOMOABOMOA YAIKUMBA KLINIKI YA REGENCY

Bomoabomoa ya Manispaa ya Ilala inayoendelea katikati ya Jiji la Dar es Salaam imeikumba kliniki ya Regency Satellite iliyoko mtaa wa Kisutu na kusababisha taharuki kwa wagonjwa waliokuwa kwenye kliniki hiyo.

Akizungumza na mwandishi, daktari wa kliniki hiyo, Mohamed Dada, alisema mgambo wa Manispaa ya Ilala walivamia eneo hilo majira ya saa nane usiku na kuanza kubomoa viambaza vyote vilivyoko mbele ya maduka bila kujali hospitali.
Alisema ubomoaji huo umeathiri kwa kiwango kikubwa huduma zilizokuwa zikitolewa kwenye kliniki hiyo ikiwemo huduma ya X ray, kuharibika kwa mifumo ya viyoyozi na mfumo wa teknolojia ya habari na mawasiliano IT kwenye kituo hicho.
Aidha, alisema kuvunjwa kwa kiambaza cha zahanati hiyo kutasababisha mvua ikinyesha maji mengi kuingia ndani hivyo kusababisha usumbufu mkubwa kwa wagonjwa na wahudumu waliopo kwenye kliniki hiyo.
Alisema mabati hayo ya kuzuia mvua katika jengo hilo linalomilikiwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC),  yako tangu mwaka 1937 na hayajawahi kuleta shida yoyote kwa kuwa yanatumika kukinga maji yasiingie kituoni hapo na wala hakuna shughuli ya biashara inayofanyika chini ya mabati hayo.
Naye Mwenyekiti wa Regency Medical Center, Dk Rajni Kanabar, aliomba serikali wakati wa kutekeleza operesheni kama hizo siku zijazo iwe inatoa tahadhari mapema ili wafanye maandalizi na kuepusha mshtuko unaoweza kuwapata wagonjwa waliopo.

No comments: