SITTA AAHIDI BUNGE LA MARIDHIANO, KUPAMBANA NA WAPINGA MUUNGANO...

KUSHOTO: Sitta akipiga kura jana. KULIA: Sitta akiwashukuru wajumbe kwa kumchagua.
Mwenyekiti mteule wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta ameonesha wazi kuwa ataongoza Bunge hilo kwa maridhiano, baada ya kueleza kundi lililokuwa nyuma yake wakati wa kampeni.

Miongoni mwa wajumbe wa kundi hilo ni mashekhe, maaskofu, wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka Zanzibar na wajumbe kutoka kundi la 201, ambao wameteuliwa na Rais.
Mbali na kundi hilo, pia Sitta ameweka bayana kuwa taarifa kwamba alikuwa na msuguano na mmoja wa waliokuwa wakiwania nafasi hiyo kupitia CCM, Andrew Chenge, si za kweli kutokana na historia yake na Mwanasheria huyo Mkuu wa Serikali wa zamani.
Hata hivyo, wakati akiweka wazi nyuma ya kampeni na ushindi wake, kulikuwa na wajumbe kutoka makundi makubwa katika Bunge hilo, na kwamba hata CCM ilimkubali kwa kauli moja,  ametangaza kuwa atawashughulikia wajumbe wenye nia ya kuvunja Muungano.
Sitta aliyechaguliwa jana kwa kura ya siri na wajumbe hao na kuibuka na ushindi wa asilimia 86.5 ya kura zote zilizopigwa, pia aliweka wazi kuwa atageuza sura mbaya ya Bunge hilo katika jamii, kwamba ni Bunge la posho na kuwa Bunge la kazi ambayo itawaridhisha wananchi kiasi cha kuwakubalia wapate kiinua mgongo.
"Nitawapenda wote nitakaowasimamia na tutamaliza Katiba katika muda uliopangwa na wananchi wajue hatupo hapa kwa posho na nitawasimamia hata tukiondoka hapa, tuondoke na kiinua mgongo," alisema.
"Humu ndani kuna vichwa ambavyo Rais (Jakaya Kikwete) amewateua na kila aliye humu ni kiongozi, isipokuwa kuna wachache ambapo tumeshawaona na kwa kujua msimamo wangu juu ya Muungano, wanataka uvunjike miye kwa busara tutawashughulikia ipasavyo.
"Tayari hao wameshasambaza tangu jana (juzi) taarifa kuwa nimezimia naumwa, wajue nitawashughulikia humu ndani ya Bunge," alisema Sitta.
Akiomba kura za wajumbe, Sitta alisema yeye ni muumini wa viwango na kasi, hivyo ataliendesha Bunge kwa viwango bora na kasi ya kupatikana Katiba kwa wakati uliopangwa.
Akijibu swali la Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugora aliyehoji katika maelezo ya Sitta anaeleza ataendesha Bunge kwa kasi na viwango, Sitta alisema; "viwango na kasi ni falsafa yangu ya kufanya kazi wananchi watatuelewa Katiba ikiwafikia katika muda uliopangwa." 
Alisema akiwa Mwenyekiti wa Bunge hilo, hatokuwa na upendeleo, mtetezi hodari wa shughuli zote zinazowafanya wajumbe wakae vizuri wawapo Dodoma na kusimamia kanuni.
Kabla ya kuanza kupigiwa kura, Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde katika swali lake kwa Sitta, alisema: "Bunge tunakwenda kuandika KatibaƊ mpya na kuna makundi mbalimbali na mwenendo wa kupitisha kanuni hasa vifungu vya 37 na 38 tumeona kutofautiana, sasa endapo katikati ya mchakato tukashindwa kuelewana na ikaelekea Bunge kuvunjika utafanyaje?"
Sitta alijibu: "Mungu aepushie mbali kushindwa kuelewana hadi Bunge livunjike, Watanzania hawatarajii kufikia huko kwa msaada wa Mwenyezi Mungu nitajitahidi tupate Katiba."
Sitta mwenye miaka 72 ambaye amekuwa mbunge kwa miaka 29 na waziri kwa miaka 14, alisema kumrejesha kwenye kiti hicho cha kuwa Mwenyekiti wa Bunge ni sawa na kumrejesha chura kwenye dimbwi la maji alilolizoea ambapo ataogelea bila matatizo.
Baada ya kumaliza kutoa neno na kujibu maswali ya wajumbe, Sitta alirudi katika kiti chake, lakini kabla ya kukaa, aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, alinyanyuka katika kiti chake na kwenda kumpongeza kwa kumshika mkono.
Baada ya kuchaguliwa, Sitta alitangaza kwamba hana uhasama na aliyekuwa akiwania kuteuliwa na CCM kugombea nafasi hiyo, Andrew Chenge.
Akitoa shukrani baada ya kuchaguliwa kushika wadhifa huo kwa kura kwa 487 kati ya 563, Sitta alisema familia yake na ya Chenge  ni marafiki wa karibu ila wamekuwa wakichonganishwa na wapambe.
"Kweli wapambe ni nuksi, kumekuwa na maneno kwamba tulikuwa na mchuano mkali ndani ya CCM na tena wa uhasama, jambo ambalo sio kweli," alisema Sitta.
Sitta alisema wakati akiwa Waziri wa Sheria mwaka 1993, ndiye aliyempendekeza Chenge kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa Rais wa Awamu ya Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi pamoja na Felix Mrema kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Alisema tangu wakati huo wamekuwa na uhusiano wa karibu, lakini kwa vile wapambe ni nuksi, ili mambo yao yaenda vizuri, lazima wavumishe mambo ambayo alisema sio mazuri.
Sitta baada ya kuchaguliwa alisema ataanda hotuba ambayo itaeleza mikasa ya mchana na usiku wakati wa kampeni yake ya kuwania nafasi hiyo ya uenyekiti, lakini alikiri kuwa alikuwa na timu nzito ya mashekhe, maaskofu, watu kutoka Zanzibar na watu wa rika mbalimbali kutoka kundi la wajumbe 201.
Alisisitiza kuwa atakuwa Mwenyekiti ambaye atahakikisha Katiba itakayopatikana inawatetea wanyonge na Katiba ambayo itailazimu Serikali ijayo kutunga sheria ambazo zitaondoa dhuluma ndani ya jamii na itatoa haki kwa wakulima, wavuvi na watu ambao hawana sauti.
Mpinzani wake Hashimu Rungwe alipata kura 69 na kura saba ziliharibika. Rungwe akitoa shukrani aliwaeleza wajumbe hao kuwa wale ambao hawakumwamini anaamini siku nyingine watamwamini na watampa kura za kutosha.
Sitta kwa upande wake alimshukuru Mungu kwa kumfungulia milango ya uongozi ndani ya Bunge hilo: "Naamini kuwa Mungu ndiye anayefungua milango ya uongozi, kwani mtu akilazimisha anaweza kupitia dirishani jambo ambalo sio jema."

No comments: